Kang'ata hajali kung'atuliwa kwa 'kusema ukweli'

Kiranja wa wengi katika seneti Irungu Kangata akizungumza katika majengo ya bunge January 11, 2021.
Kiranja wa wengi katika seneti Irungu Kangata akizungumza katika majengo ya bunge January 11, 2021.
Image: EZEKIEL AMING'A

Kiranja wa wengi katika seneti Irungu Kang’ata amesema hang’atuki ng’oo na kushikilia msimamo wake kwamba watu wengi katika eneo la Mt Kenya hawaungi mkono BBI na kwamba hajali kama msimamo huo utapelekea yeye kuvuliwa wadhifa wake.

Akihutubia wanahabari katika majengo ya bunge siku

ya Jumatatu, Kang’ata alisema kwamba BBI inakabiliwa na changamoto za kisiasa katika eneo la Mt Kenya ambazo zinahitaji kushughulikiwa.

Na katika kile ambacho huenda kikwaza mrengo wa rais Uhuru Kenyatta kuhusu BBI, Kang’ata ameshikilia msimamo wake wa kuunga mkono pendekezo la naibu rais William Ruto kuruhusu wakenya kupigia kura vipengele mbali mballi katika msuada wa BBI ili kuondoa tishio la msuada huo kuangushwa katika kura ya maamuzi.

Seneta huyo wa Murang’a hata hivyo alisema kwamba barua yake kwa  rais Uhuru Kenyatta ilikuwa kwa nia njema na kukariri msimamo wake kumuunga mkono rais Kenyatta licha ya rais kupuuzilia mbali barua yake.

Kang’ata alisema dhana kuwa mchakato wa BBI ulikuwa ukisukumwa na mrengo mmoja wa chama cha Jubilee na kutumia maafisa wa utawala wa mkoa kumeathiri umaarufu wa BBI katika eneo hilo.

Alishikilia kwamba alitoa maoni yake baada ya kukutana na wenyeji, viongozi wenye ushawishi na wataalam kutoka Murang’a  ambao walionyesha shauku kuhusu BBI.

Alisema kwamba alikuwa na jukumu la kuambia serikali ukweli na kumkashifu kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Amos Kimunya kwa kumdhalilisha na kukosa kumwambia rais ukweli.

Kang’ata hata hivyo alikwepa swali ikiwa anapanga kuhama mrengo wa kieleweke na kujiunga na ule wa naibu rais ‘Tanga tanga’ akisema kwamba ni kiranja wa Jubilee na haamini kwa migawanyiko katika uongozi wake.