Raila aunga mkono azimio la Joho kuwania urais - 2022

Kinara wa ODM Raila Odinga na naibu wake Hassan Joho
Kinara wa ODM Raila Odinga na naibu wake Hassan Joho
Image: JOHN CHESOLI

Kila mtu ana haki ya kugombea urais, kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga amesema.

Akizungumza katika kaunti ya Mombasa siku ya Jumatano, Raila alisema kuwa anaunga mkono kila mtu ndani ya ODM ambaye anataka kugombea urais wa 2022.

"Baada ya kila mwaka tuna uchaguzi na viti vinabaki wazi. ODM ni chama cha kitaifa na watu wana uhuru wa kuwania nyadhifa," alisema Raila.

"Joho ni naibu kiongozi wa chama, wana haki ya kugombea kiti chochote na kila Mkenya ana haki sawa. Ni chama cha ODM ambacho kitaamua ni nani atakayepeperusha bendera. Ninaunga mkono azma ya Joho ya urais."

Gavana wa Mombasa Hassan Joho alisema atawania urais katika uchaguzi wa 2022 na kwamba azimio lake haliwezi kuzuilika. Joho alisema tayari amewasilisha nyaraka zake za uteuzi kwa chama cha ODM na anatarajia kuungwa mkono kabisa na vinara akiwemo kiongozi Raila Odinga iwapo atashinda mchujo.

“Nimesikia watu wakihoji uwezo wangu. Ikiwa hawawezi kushinda kiti cha juu, basi hilo ndio shida yao. Kwa upande wangu, sitaacha kitu kingine chochote isipokuwa urais, ”Joho alisema.

Katika ziara yake ya Pwani, Raila alipuuzilia mbali baadhi ya viongozi wa Pwani wanaoshinikiza kubuniwa kwa chama cha kanda hiyo akisema hatua hiyo ni tishio kwa umoja wa kitaifa.

Alisema viongozi wanapaswa kuzingatia tu kuboresha uchumi wa eneo la pwani ili kunufaisha wakazi wote na sio mkataba wa kikanda.

Baadhi ya magavana na wabunge wa mrengo wa ODM wanashinikiza kuundwa kwa chama cha kisiasa cha wa pwani. Viongozi hao, wakiongozwa na Gavana wa Kilifi Amason Kingi ambaye kwa miaka mingi amekuwa mtetezi sugu wa ODM walisema kwamba wakati umewadia kwa eneo la Pwani kuondoka ODM na kujiunga na siasa za kitaifa kupitia chama chao.

Raila alizidi kuonya viongozi dhidi ya kutumia vibaya demokrasia ya vyama vingi kuunda vyama vya siasa vya kikabila.