Mudavadi ataka serikali kufafanulia Wakenya hitaji la mkopo wa IMF

Muhtasari

• Mikopo ya IMF kwa kawaida huambatana na masharti mengi ambayo serikali hulazimika kuyatimiza.

• Mudavadi siku ya Jumatano alisema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa serikali kuwaelezea wananchi ni hatua zipi zitakazochukuliwa kama hitaji kuu kuhusiana na mkopo huo.

Kinara wa ANC Musalia Mudavadi. Picha:HISANI
Kinara wa ANC Musalia Mudavadi. Picha:HISANI

Serikali imetakiwa kuweka bayana mipango iliyochochea mkopo wa hivi punde wa shirika la fedha duniani - IMF.

Kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi, ambaye wakati mmoja aliwahi kuhudumu kama waziri wa fedha, ameitaka serikali kufafanua zaidi mikakati  ambayo itaangaziwa kwenye msukumo huu mzima wa mkopo unaofadhiliwa na shirika la kifedha la IMF.

Mudavadi siku ya Jumatano alisema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa serikali kuwaelezea wananchi ni hatua zipi zitakazochukuliwa kama hitaji kuu kuhusiana na mkopo huo.

Alisema ufafanuzi huu utawatayarisha wakenya iwapo kutakuwa na mabadiliko yeyote katika sekta ya umma au ile ya kibinafsi ndiposa wakenya wasiwekewe masharti ambayo huenda yakawapata kwa mshangao.

Mikopo ya IMF kwa kawaida huambatana na masharti mengi ambayo serikali hulazimika kuyatimiza.

Kuna habari kwamba tayari shirika la IMF limethibitisha kuwa ni lazima Kenya itimize mahitaji yanayokusudiwa kwenye mpangilio huu wa mkopo ambao Mudavadi anasema kuwa una umuhimu mkubwa kuisaidia Kenya sio tu kukabiliana na janga la Corona bali pia kwenye mikakati yake ya kuratibu vile madeni ya kitaifa yatalipwa.

Kwa kawaida mikopo ya IMF huambatana na masharti makali.