Aliyekuwa mkufunzi wa Raga Benjamini Ayimba aomba msaada kugharamia matibabu

Muhtasari

• Familia ya Ayimba imetoa wito kwa wahisani kujitokeza kuwawezesha kulipia ada za matibabu za shujaa huyo ambayo kufikia sasa imetimia shilingi milioni mbili na inazidi kuongezeka.

Benjamin Ayimba
Benjamin Ayimba
Image: HISANI

Aliyekuwa mkufunzi wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande Benjamin Ayimba amelazwa na anahitaji msaada wako kulipia garama za matibabu.

Familia ya Ayimba imetoa wito kwa wahisani kujitokeza kuwawezesha kulipia ada za matibabu za shujaa huyo ambayo kufikia sasa imetimia shilingi milioni mbili na inazidi kuongezeka.

Ayimba amekuwa ndani na nje ya hospitali tangu mwishoni mwa mwaka jana alipogunduliwa kuugua Malaria ya ubongo.

Muungano wa mchezo wa raga nchini katika taarifa yake ulisema kwamba hali ya Ayimba imezidi kudhoofika na kutoa wito kwa wahisani kujitokeza kumchangia pesa kupitia PAYBILL NUMBER  8021673. jina: BENJAMIN OTIENO AYIMBA MEDICAL.

Ayimba aliongoza kikosi cha taifa cha raga kushinda taji la kwanza la Rugby Sevens nchini Singapore mwaka 2016 kwa kulaza mabingwa watetezi Fiji alama 30-7 katika fainali.

Anaendelea kupokea matibabu katika Nairobi Hospital ambako amekuwa kwa majuma matatu sasa.