Mwanahabari Betty Barasa azikwa leo

Muhtasari

• Betty aliuawa siku ya Jumatano usiku wiki iliyopita kwa kupigwa risasi nyumbani kwake na watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki.

Marehemu Betty Barasa
Betty Barasa Marehemu Betty Barasa
Image: Maktaba

Mwanahabari wa KBC Betty Barasa aliyeuawa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake mtaani Ngong anazikwa leo katika boma lake eneo la Ololua, Ngong.

Betty aliuawa siku ya Jumatano usiku wiki iliyopita kwa kupigwa risasi nyumbani kwake na watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki.

Marehemu alikuwa mhariri wa video katika idhaa ya kitaifa KBC na alivamiwa na watu waliokuwa wamemngojea punde tu alipowasili nyumbani kwake mwendo wa saa mbili unusu jioni.

 Alikuwa amekuwa kazini na kuelekea katika nyumba yake mpya akitarajia kujiunga na mumewe na watoto wake watatu.

Alikuwa tu amehamia katika nyumba hiyo.

Polisi wanaendelea na uchunguzi kubaini kilichopelekea mauaji ya mwanahabari huyo kwa sababu wauaji wake waliiba tu simu na tarakilishi kabla ya kutoroka. Simu moja waliokuwa wameiba ilipatikana mita chache kutoka nyumbani kwake.

Baraza la vyombo vya habari nchini (MCK) lilitoa wito kwa idara ya polisi kufanya uchunguzi wa kina kuwapata waliohusika katika mauaji hayo.