Masaibu ya kuwa mkenya! Bei za mafuta zatarajiwa kupanda tena

Muhtasari

• Lita moja ya dizeli inatarajiwa kuongezeka hadi Shilingi 114.56 kutoka Shilingi 107.66 ya sasa, ikiashiria kupanda kwa takriban shilingi 7.

Image: MAKTABA

Bei ya mafuta huenda ikapanda katika bei mpya za kila mwezi kutangazwa leo na mamlaka ya kudhibiti kawi nchini (EPRA).

Duru katika Mamlaka ya Udhibiti wa kawi na petroli (EPRA) zilidokeza kwamba bei ya lita moja ya petroli huenda ikapanda kwa angalau Shilingi 6, ikisukuma bei ya wastani kuwa angalau Shilingi 128.87 kwa lita ya mafuta ya petroli.

Lita moja ya dizeli inatarajiwa kuongezeka hadi Shilingi 114.56 kutoka Shilingi 107.66 ya sasa, ikiashiria kupanda kwa takriban shilingi 7.

 

Mafuta ya taa yanayotumiwa zaidi katika maeneo ya mashambani na makazi yasiyokuwa rasmi kwa ajili ya mwangaza na upishi yanatarajiwa kupanda hadi shilingi 100 kutoka Shilingi 97.85.

Kuongezeka kwa bei inayotarajiwa kuanza kutumika Aprili 15 hadi Mei 14 kunachangiwa na kupanda kwa gharama ya mafuta yasiyosafishwa kutoka nje.

Hili litakuwa ongezeko la nne mfululizo mwaka huu. Bei ya petroli, dizeli, na mafuta ya taa iliongezeka kwa Shilingi 8.19 kwa lita, Shilingi 5.51 kwa lita, na Sh5.32 kwa lita, mtawaliwa mwezi Februari.

Mwezi Januari, bei za petroli, dizeli na mafuta ya taa ziliongezeka kwa Shilingi 0.17, 4.57 na 3.56 kwa lita mtawaliwa.

Bei ya juu ya mafuta yasiyosafishwa mwezi Machi na Aprili imesababishwa na uzalishaji wa chini wa mafuta ghafi.

Katika bei zilitangazwa mwezi Machi na ambazo zinamalizika leo usiku Super petroli ilipanda kwa Shilingi 7.63 hadi 122.81 kwa lita. Bei za dizeli na mafuta ya taa, zilipanda kwa Shilingi 5.75 na 5.41 kwa lita mtawaliwa.

Utathmnini wa kina umebaini kuwa zaidi ya asilimia 50 ya bei ya reja reja ya mafuta kwa lita ni ushuri jwa serikali.  

 

Wakenya hulipa angalau kodi tisa tofauti kwa mafuta, ushuru wa juu zaidi katika eneo la Afrika Mashariki.