Mahakama yaongeza makataa ya utekelezwaji wa ada mpya za maegesho Nairobi

Muhtasari

• Jaji Anthony Mrima ameamuru shirika la NMS lijumuishwe katika kesi hiyo kama mmoja wa wahusika.

• Kaunti ya Nairobi ilitoa ilani ya umma ya Desemba 2, mwaka jana kuongeza ada za maegesho kutoka Shilingi 200 hadi Shilingi 400.

• Ada hizo mpya zingeanza kutekelezwa Desemba 4, 2020.

Askari wa jiji la Nairobi wakifungia gari ambalo halikuwa limelipiwa maegesho
Askari wa jiji la Nairobi wakifungia gari ambalo halikuwa limelipiwa maegesho
Image: MAKTABA

Mahakama kuu imeongeza maagizo ya kuzuia Serikali ya Kaunti ya Jiji la Nairobi kuongeza ada ya kuegesha magari ya kibinafsi na magari ya utumishi wa umma kutoka Shilingi 200 hadi 400.

Jaji Anthony Mrima ameamuru shirika la NMS lijumuishwe katika kesi hiyo kama mmoja wa wahusika.

Jaji aliamuru tarehe ya kutajwa ya Mei 3, 2021, ili kuruhusu wahusika kuwasilisha maoni yao na kwa maagizo zaidi.

Mwezi Machi jaji pia aliongezea amri.

Kupitia kwa Wakili Henry Kurauka, Cofek na Chama cha Wamiliki wa Matatu walisema kwamba nyongeza ya ada haikuwa ya haki, isiyo na busara na haikushirikisha umma kulingana na Kifungu cha 10 cha Katiba.

Ada hizo mpya zingeanza kutekelezwa Desemba 4, 2020.

Kaunti ya Nairobi ilitoa ilani ya umma ya Desemba 2, mwaka jana kuongeza ada za maegesho kutoka Shilingi 200 hadi Shilingi 400.

Mabasi ambayo sio magari ya huduma za umma yalipaswa kulipa Shilingi 1,000 kila siku.

Ilani hiyo ilitiwa saini na mkurugenzi wa huduma za maegesho katika kaunti ya Nirobi Tom Tinega.

Cofek ilipinga uamuzi huo ikisema utaumiza watumiaji wanaotafuta huduma za uchukuzi na maegesho ndani ya eneo hilo.