Uhuru amtimua Kembi Gitura kutoka bodi ya KEMSA

Muhtasari

• Rais Uhuru Kenyatta amefutilia mbali uteuzi wa Kembi Gituri kuhudumu katika bodi ya shirika la Kemsa.

• Badala yake rais Kenyatta amemteua Mary Mwadime kuwa mwenyekiti wa bodi hiyo.

Aliyekuwa mwenyekiti wa Kemsa Kembi Gitura
Aliyekuwa mwenyekiti wa Kemsa Kembi Gitura
Image: MAKTABA

Rais Uhuru Kenyatta amefutilia mbali uteuzi wa Kembi Gituri kuhudumu katika bodi ya shirika la Kemsa.

Badala yake rais Kenyatta amemteua Mary Mwadime kuwa mwenyekiti wa bodi hiyo.

Katika ilani ya Gazeti rasmi la serikali nakala ya Aprili, rais alisema kwamba muhula wa Mwadime ofisini utaanza Aprili 30 kwa kipindi cha miaka mitatu.

Kupigwa kalamu kwa Gitura kunafuatia kashfa ya ununuzi inayokumba shirika la Kemsa.

Mwezi uliopita, wabunge walielezea wasiwasi kuhusu uteuzi wa Gitura kwa Mamlaka ya Mawasiliano.

Kamati ya bunge chini ya uwenyekiti wa mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir ilisema uteuzi wa seneta huyo wa zamani wa Murang’a haufanywa kwa nia nzuri ikizingatiwa uchunguzi wa kashfa ya Kemsa unaoendelea.

Katika ilani iyo hiyo, Waziri wa afya Mutahi Kagwe ameteua wanachama wapya kwenye bodi ambao watahudumu kwa kipindi cha miaka mitatu, kuanzia Aprili 30, 2021.

Wanachama hao ni pamoja na Lawrence Wahome, Robert Nyirangu, Terry Kiunge Ramadhani na Linkon Nyaga Kinyua.