Kenya yatoa agizo la karantini ya siku 14 kwa wasafiri kutoka UK

Muhtasari

• Nchi zingine ni pamoja na; Brunei, Jamhuri ya Czech, Kuwait, Pakistan na Thailand.

 
• Wale wanaosafiri kutoka nchi hizi wanapaswa kuwa wamepimwa na kupatikana bila virusi vya Covid-19, vipimo vinafaa kuwa vimefanywa ndani ya saa 96 kabla ya kusafiri.

Image: MAKTABA

Kenya imetoa agizo la kuwekwa karantini ya lazima ya siku 14 kwa wasafiri wote wanaowasili kutoka nchi sita pamoja na Uingereza.

Katika taarifa yake, Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Kenya ilisema ndege zote za abiria, iwe ya kibiashara au ya kukodisha, kati ya Kenya na Uingereza, zitasitishwa.

Nchi zingine ni pamoja na; Brunei, Jamhuri ya Czech, Kuwait, Pakistan na Thailand.

Wale wanaosafiri kutoka nchi hizi wanapaswa kuwa wamepimwa na kupatikana bila virusi vya Covid-19, vipimo vinafaa kuwa vimefanywa ndani ya saa 96 kabla ya kusafiri.

"Raia wote wa Uingereza na wakaazi wanaosafiri kwenda Kenya kutoka Uingereza kupitia njia yoyote ambao wana vipimo halali vya Covid-19, lakini hawana yveti halali vya  chanjo ya Covid-19, watawekwa chini ya karantini ya siku 14 za lazima," ilisema taarifa hiyo.

Wasafiri watatengwa kwa gharama yao wenyewe.

"Wasafiri wote chini ya umri wa miaka 18 watahitaji tu cheti cha kupimwa Covid-19 pekee kuingia Kenya," KCAA iliongeza.

Mwishoni mwa wiki, Wakenya walihimizwa kuwa macho wakati serikali inaendelea na mpangilio wa kufuatilia aina mbali mbali za Covid-19 katika juhudi za kudhibiti aina mpya za Covid-19 nchini.

Wizara ya Afya ilithibitisha kuwa aina kubwa ya virusi vya corona nchini ilikuwa kutoka nchi ya Uingereza, ambayo pia inajulikana kama B.1.1.7.

Aina ya Uingereza na ile ya Afrika Kusini imekuwa ikizunguka nchini tangu Januari na sampuli zilizochukuliwa kwa mpangilio kutoka Nairobi na kaunti jirani zimeonyesha wale waliopatikana na aina hiyo hawakuwa na historia ya kusafiri.

Ingawa sio hatari sana kama aina ya asili ya virusi vya Covid-19, inaambukiza sana na inaweza kupitishwa kwa haraka.

Wiki iliyopita, Kenya ilithibitisha visa kadhaa vya aina kali ya India coronavirus kutoka kwa wasafiri.

Mwezi uliopita, Uingereza ilipiga marufuku abiria wanaosafiri kutoka Kenya kuingia katika nchi hiyo kuanzia Aprili 9 ili kuzuia kuenea kwa Coronavirus.