OCS wa Kileleshwa kufika mahakamani kwa madai ya kuteswa kwa mshukiwa

Muhtasari

• Mshukiwa alieleza mahakama kwamba alipigwa na polisi ambao walikuwa wakimpeleka kortini.

 

Mshukiwa Moses Amwayi akiwa katika mahakama ya Kibera
Mshukiwa Moses Amwayi akiwa katika mahakama ya Kibera

Mahakama ya Kibera imemuagiza OCS wa Kileleshwa kufika mbele yake baada ya mshukiwa wa ulanguzi wa bangi kudai kuteswa na kuzuiliwa kupita muda unaotakikana kisheria.

Hakimu mkuu wa Kibera Joyce Gandani siku Alhamisi aliita OCS baada ya mtu anayetuhumiwa kusafirisha misokoto 36 ya bhang yenye thamani ya shilingi 720 kuambia mahakama kwamba alikamatwa siku ya Jumatatu na kushtakiwa Alhamisi kinyume cha sheria.

Moses Amwayi, mhudumu wa bodaboda, mwenye umri wa miaka 19 hata hivyo alikanusha mashtaka ya ulanguzi wa bangi na akaomba apewe kifungo rahisi.

Kupitia wakili wake Julie Soweto, Amwayi alidai kwamba alipelekwa kortini mapema wiki hii lakini hakuwahi kufikishwa mbele ya kortini badala yake alifungiwa ndani ya gari huku washukiwa wengine wakishtakiwa.

Mshukiwa alieleza mahakama kwamba alipigwa na polisi ambao walikuwa wakimpeleka kortini.

Kulingana na stakabadhi za kesi, alitenda kosa hilo mnamo Mei 17 katika kituo cha bodaboda mtaani Kawangware ambapo alipatikana na bangi hiyo.

Hakimu Gandani alimuachilia kwa dhamana ya shilingi 50,000 na hakikisho au dhamana ya pesa taslimu ya shilingi 5000.

Aliagiza kesi hiyo kutajwa mnamo Juni 14 wakati polisi watajibu madai ya mateso.