UONGOZI WA JUBILEE

"Wakati wa mabadiliko uongozini wa Jubilee umefika" Kinyajui

Gavana Lee Kinyajui azungumzia masikitito yake kutokana na masaibu yanayoendelea kukumba chama cha Jubilee

Muhtasari

•Gavana Lee Kinyajui azungumzia masikitito yake kutokana na masaibu yanayoendelea kukumba chama cha Jubilee

•Amekashifu kitendo cha kuwateua wagombeaji kutokana na uhusiano au kuzingatia hisia ama mapato ya kiuchumi.

lee kinyajui
lee kinyajui
Image: Hisani

Gavana wa kaunti ya Nakuru, Lee Kinyajui ameeleza masikitito yake kutokana na masaibu yanayoendelea kukumba chama cha Jubilee.

Kupitia ujumbe aliochapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook, Kinyajui ameeleza kuwa wananchi wamekuwa wakinyimwa shaki za kidemokrasia kwenye uteuzi wa wagombeaji viti kwa tikiti ya Jubilee na hilo kusababisha wao kulipiza kisasi kwa kutowachagua wanaoteuliwa.

“Kwenye uchaguzi ndogo zilizofanyika hivi majuzi, ahadi yetu ya kushikilia matakwa ya wananchi na heshima ya haki za kidemokrasia katika uteuzi wa wagombeaji zimekiukwa na hilo limesababisha kuteuliwa kwa wagombeaji wasio na umaarufu” Kinyajui ameeleza.

Kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika katika maeneo ya Juja, Bonchari na Rurii siku ya Jumanne, chama cha Jubilee hakikupata ushindi wowote licha ya kuwa na wagombea viti katika kila eneo. Jambo ambalo limeibua gumzo sana ikikisiwa kuwa huenda chama hicho kimepoteza umaarufu wake.

Kinyajui amesisitiza kuwa ni sharti mabadiliko yafanyike katika uongozi wa chama cha Jubilee huku akisema kuwa chama hicho kimejazwa na watu wengi ambao hawaongezei thamana yoyote kwenye chama.

“Tunaamini wakati wa kutekeleza mabadiliko katika uongozi wa chama umefika. Yafaa tuingize wau wapya ili tufufue ndoto za kuungwa mkono kwa chama” Kinyajui alisema.

Gavana huyo amekashifu kitendo cha kuwateua wagombeaji kutokana na uhusiano au kuzingatia hisia ama mapato ya kiuchumi huku akisema kuwa hiyo ni sawa na kujichimbia kaburi.