Jaji mkuu: Martha Koome kuapishwa leo

Muhtasari

• Rais Uhuru Kenyatta siku ya Jumatano alimteua Martha Koome kuwa jaji mkuu baada ya bunge kumuidhinisha siku iyo hiyo.

• Jaji Martha Koome atakuwa mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa huo katika historia ya Kenya.

• Kulingana na sheria jaji mkuu anafaa kuhudumu kwa kipindi cha miaka 10 au anapofikisha umri wa miaka 70 kulingana na kile kitakachojiri mwanzo.

Jaji Martha Koome
Jaji Martha Koome
Image: JSC

Jaji wa mahakama ya rufaa Martha Koome anaapishwa leo Ijumaa kuwa jaji mkuu wa Kenya kuchukuwa nafasi ilioachwa wazi na David Maraga aliyestaafu mwezi Disemba mwaka jana.

Rais Uhuru Kenyatta siku ya Jumatano alimteua Martha Koome kuwa jaji mkuu baada ya bunge kumuidhinisha siku iyo hiyo.

Spika Justin Muturi aliitisha kikao maalum kujadili uteuzi wa Koome kupitia arifa ya Gazeti rasmi la serikali siku ya Jumatatu wiki hii.

Kamati ya bunge ya haki na maswala ya kisheria iikuwa imeidhinisha uteuzi wa Martha Koome baada ya jina lake kuwasilishwa kwa bunge na rais Kenyatta.

"Bunge hili linakubali uteuzi wa Koome kwa wadhifa wa Jaji mkuu," kamati ya bunge lisema katika ripoti yake.

Wakati wa mahojiano yake, Koome aliahidi kurejesha maelewano na kumaliza uhasama kati ya idara ya mahakama na bunge.

Koome alikuwa ameonya maafisa wafisadi katika idara ya mahakama na kwamba atatoa mifano kuwa vielelezo kwa maafisa wengine.

Jaji Martha Koome atakuwa mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa huo katika historia ya Kenya. Jaji huyo mwenye umri wa miaka 61 anatarajiwa kuhudumu katika wadhifa huo kwa takriban miaka tisa.

Kulingana na sheria jaji mkuu anafaa kuhudumu kwa kipindi cha miaka 10 au anapofikisha umri wa miaka 70 kulingana na kile kitakachojiri mwanzo.