Washukiwa 2 wauawa huku polisi wakimuokoa mhubiri aliyetekwa nyara

Muhtasari

• John Dinguri Chege, alitekwa nyara saa nne usiku na watu wanne waliokuwa wamejihami, alipokuwa akienda nyumbani.

• Kulingana na polisi, bastola aina ya Smith na Wesson zikiwa na risasi na kisu, vilipatikana kutoka kwa washukiwa.

• Msako unaendelea kuwatafuta washukiwa wawili waliotoroka.

crime
crime

Mchungaji mwenye umri wa miaka 57 katika Kanisa la Kiangalikana eneo la Kabete kaunti ya Kiambu usiku wa Alhamisi aliokolewa kutoka kwa genge lenye silaha lililokuwa limemchukua mateka.

Polisi walisema washukiwa wawili waliuawa kwa kupigwa risasi katika oparesheni kali ya kumuokoa.

Bastola na silaha nyingine zilipatikana kutoka kwa washukiwa.

Kulingana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, kasisi huyo aliyetambuliwa kwa jina la John Dinguri Chege, alitekwa nyara saa nne usiku na watu wanne waliokuwa wamejihami, alipokuwa akienda nyumbani.

Baada ya kudhibiti gari lake, majambazi waliiamuru kuelekea eneo la Kiamumbi katika kaunti ya Kiambu.

Wakati maafisa wa polisi walipopata habari za tukio hilo, waliwafuata washukiwa huku maafisa wengine wakiweka mtego katika kando ya Barabara ya Kamiti, karibu kilomita 20 kutoka eneo la utekaji nyara.

Kulingana na polisi, katika oparesheni iliopangwa na kutekelezwa kwa njia nzuri kumwokoa mhudumu huyo wa Mungu, gari hilo lilikamatwa mita kadhaa kutoka eneo la Jacaranda karibu na Kiamumbi.

Washukiwa waliamriwa kujisalimisha lakini walikaidi maagizo hayo, na kupelekea ufyatulianaji wa risai na majambazi wawili kuuawa.

Washukiwa wengine wawili walitoroka wakiwa na majeraha ya risasi, wakimuacha mchungaji.

Kulingana na polisi, bastola aina ya Smith na Wesson zikiwa na risasi na kisu, vilipatikana kutoka kwa washukiwa.

Msako unaendelea kuwatafuta washukiwa wawili waliotoroka. Polisi walisema wanachunguza kubaini sababu ya mchungaji huyo kulengwa.

“Lazima kuna kitu walikuwa wakifuata. Tunataka kubaini nia yao, ”afisa mmoja anayeshiriki uchunguzi huo alisema.