Wandani wa Ruto waonya dhidi ya ubaguzi katika vita dhidi ya ufisadi

Muhtasari

• Mbunge wa Kandara Alice Wahome alisema ubaguzi na mapendeleo vinaathiri vita dhidi ya ufisadi nchini.

• Seneta wa Nakuru Susan Kihika alimtaka DCI kuacha kutumiwa kuafikia malengo ya kisiasa.

Naibu rais William Ruto
Image: Maktaba

Wabunge wanaoegemea mrengo wa Naibu Rais William Ruto wamesema vita dhidi ya ufisadi haifai kuwa ya kisiasa.

Walisema kuwa idara za serikali zilikuwa zikitumia vita dhidi ya ufisadi kuzima sauti huru.

Walitaja idara ya DCI kama mhusika mkuu katika vitisho kwa viongozi wanaohusishwa na naibu rais.

Viongozi hao walijumuisha Mwakilishi wa Wanawake wa Kiambu Gathoni wa Muchomba, Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa, Mbunge wa Kandara Alice Wahome, Mbunge wa Kabete Githua Wamacukuru, Seneta wa Nakuru Susan Kihika, Mwakilishi wa Wanawake wa Nakuru Lizah Chelule, Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na Mwakilishi wa wanamke wa Taita Taveta Lydia Haika.

Wahome alisema ubaguzi na mapendeleo vinaathiri vita dhidi ya ufisadi nchini.

"Sheria lazima zitekelezwe kwa usawa bila kujali yule ambaye analengwa," alisema.

Alimshauri mwakilishi wa wanawake wa Kiambu ambaye hivi karibuni alijiunga na mrengo wa kisiasa wa Ruto kujiandaa kwa unyanyasaji kutoka kwa DCI, tume ya EACC, mamlaka ya KRA, kati ya idara zingine.

"Kesi zilizochochewa kisiasa zitakuja dhidi yako, lakini kaa imara katika msimamo wako wa kisiasa," alisema mbunge huyo wa Kandara.

Bi Kihika alimtaka DCI kuacha kutumiwa kuafikia malengo ya kisiasa.

"Huwezi kuwasilisha kesi za kubuniwa dhidi ya washirika wa Ruto. Wakati wa uovu unakwisha, ”alisema.

Alisema hawatatishwa lakini wataongeza juhudi zao kwa kuimarisha maisha ya wakenya wa kawaida.

Usemi wake uliungwa mkono na mwenzake wa Kikuyu ambaye alisema mashirika ya Serikali yalikuwa yakitumika kuwanyanyasa viongozi wengine.

"DCI na mashirika mengine ya serikali lazima yaache mateso haya ya kisiasa," alisema Kimani.

"DCI inapaswa kuzingatia kufichua wale walio shiriki wizi wa pesa za COVID-19."

"Tunaunga mkono vita dhidi ya ufisadi lakini lazima vifanyike kwa njia huru bila upendeleo wa kisiasa".