AFUENI JAGUAR

Ruto aandamana na viongozi wengine kumfariji Jaguar hospitalini

Awali siku ya Jumatano, Ruto alipatana na viongozi wa Nairobi katika maeneo ya Karen jijini Nairobi

Muhtasari

•Kupitia mtandao wa Instagram, Jaguar aliweka picha moja ambayo ilionyesha wakijadiliana na Ruto. Kwenye picha ambazo Radio Jambo imeweza kuona, naibu rais alionekana akimfariji mbunge huyo wa mara ya kwanza bungeni.

•Jaguar anaendelea kupata nafuu hospitalini baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu siku ya Jumatatu.

Ruto na viongozi wengine wakimfariji Jaguar hospitalini
Ruto na viongozi wengine wakimfariji Jaguar hospitalini
Image: Hisani

Naibu rais William Ruto alimtembelea mbunge wa Starehe, Charles Njagua Kanyi almaarufu kama Jaguar hospitalini ambako amelazwa jioni ya Jumatano.

Rutoa aliandamana na viongozi wengine ikiwemo mbunge wa Dagoretti Kaskazini John Kiarie, Nixon Korir wa Lang'ata, Mohammed Ali  'Jicho Pevu' wa Nyali, George Theuri wa Embakasi Magharibi na Yusuf Hassan  wa Kamukunji.

Kupitia mtandao wa Instagram, Jaguar aliweka picha moja ambayo ilionyesha wakijadiliana na Ruto. Kwenye picha ambazo Radio Jambo imeweza kuona, naibu rais alionekana akimfariji mbunge huyo wa mara ya kwanza bungeni.

Jaguar anaendelea kupata nafuu hospitalini baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu siku ya Jumatatu.

Video ya mbunge huye akiwa hospitalini ilionyeshwa kwa mara ya kwanza na mwanamuziki DK Kwenye Beat ambaye alifichua habari za kulazwa hospitali kwake.

Mwanamuziki wa kikundi cha P-unit Gabu alihakikishia Wakenya kuwa mwanasiasa huyo ambaye alikuwa mwanamuziki kabla ya kujitosa siasani alikuwa katika hali nzuri.

"Mhesh ako sawa sana. Mungu ni mwema mazee" Gabu alisema.

Awali siku ya Jumatano, Ruto alipatana na viongozi wa  Nairobi katika maeneo ya Karen jijini  Nairobi.

Viongozi ambao walihudhuria mkutano huo ni pamoja na seneta Millicent Omanga, mbunge wa Embakasi Magharibi George Theuri, Nixon Korir wa Lang'ata, James Gakuya wa Embakasi Kaskazini, Rigathi Gachagua wa Mathira, George Murugara wa Tharaka na aliyekuwa mbunge wa Starehe, Margaret Wanjiru.

Kupitia mtandao wa Twitter, Ruto alisema kuwa wamejitolea kuunda sera ambazo zitasaidia mamilioni ya Wakenya kupata kazi.

"Tumejitolea kuunda sera ambazo zitasaidia kupea fedha za kuanzisha  na kukuza biashara ndogo ndogo ili ziweze kustawi. Kufuatia hayo, ajira itapatika na mamilioni ya Wakenya wataweza kuwa na mapato ya kila siku.' Ruto alisema.