Mzozo wa Afghanistan: rais Ashraf Ghani atorokea UAE

Muhtasari

• Ghani alikimbia Afghanistan wakati Taliban ilipoingia katika mji mkuu Kabul mwishoni mwa wiki.

• Hata hivyo hatua yake kuondoka imekosolewa vikali na wanasiasa wengine wa Afghanistan.

Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani
Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani
Image: Maktaba

Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani yuko katika Falme za Kiarabu, taifa la Ghuba limethibitisha.

Ghani alikimbia Afghanistan wakati Taliban ilipoingia katika mji mkuu Kabul mwishoni mwa wiki.

Wizara ya mambo ya nje ya UAE ilisema nchi hiyo ilimkaribisha Bwana Ghani na familia yake kwa misingi ya kibinadamu.

Kulikuwa na uvumi kwamba Ghani angekimbilia Tajikistan. Pia kuna ripoti ambazo hazijathibitishwa kuwa alikuwa na kiasi kikubwa cha pesa wakati akitoroka.

Katika ujumbe kwa raia wa Afganistan kwenye Facebook siku ya Jumapili, Bw. Ghani alisema alifanya uamuzi mgumu kuondoka ili kuepuka umwagikaji damu katika mji mkuu.

Hata hivyo hatua yake kuondoka imekosolewa vikali na wanasiasa wengine wa Afghanistan.

"Mungu atamwajibisha na taifa pia litamhukumu," alisema Abdullah Abdullah, mwenyekiti wa Baraza Kuu la Upatanisho wa Kitaifa la Afghanistan.