ODM yavipa ANC na Wiper milioni 117.2

Muhtasari

• Fedha hizo zilikuwa sehemu ya mgao wa vyama vya siasa ambao chama hicho kilikubaliana mwezi uliopita kugawanya na washirika wake wa zamani.

• Wiper cha Kalonzo Musyoka kilipokea shilingi milioni 70.4, ANC cha Musalia Mudavadi ilipata Shilingi milioni 43.8, wakati CCM ya Isaac Ruto ikipewa shilingi milioni 3.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga
Kiongozi wa ODM Raila Odinga

ODM imetimiza ahadi yake na kutowa shilingi milioni 117.2 kwa washirika wake wa zamani katika muungano wa NASA.

ODM hata hivyo hata hivyo, imezuilia Shilingi milioni 36 za Ford Kenya ambayo inakabiliwa na malumbano ya uongozi.

Fedha hizo zilikuwa sehemu ya mgao wa vyama vya siasa ambao chama hicho kilikubaliana mwezi uliopita kugawanya na washirika wake wa zamani.

Afisa wa cheo cha juu katika ODM siku ya Jumatatu alithibitisha kwamba walihamisha pesa hizo kwa akaunti za Wiper na ANC wiki iliyopita.

“Tuliwapa pesa kama tulivyokubaliana. Kwa Ford Kenya tutashikilia, hatuwezi kutowa pesa na bado kuna mzozo wa uongozi, "afisa huyo alisema.

Image: PSCU

Wiper cha Kalonzo Musyoka kilipokea shilingi milioni 70.4, ANC cha Musalia Mudavadi ilipata Shilingi milioni 43.8, wakati CCM ya Isaac Ruto ikipewa shilingi milioni 3.

Hata hivyo, msemaji wa ANC Nathaniel Mong'are alisema hajui kuwepo kwa pesa zozote kutoka ODM.

"Kinachotakiwa kufanywa na ODM, ni kukupa taarifa ya benki inayoonyesha kuwa wametuma pesa hizo kwa akaunti za ANC. Ni wao kudhibitisha wametupa pesa, ”alisema.

Alisema madai ya ODM yanaweza kuwa tu propaganda kuonyesha kuwa chama hicho kina uaminifu.

“Ikiwa nitafanya shughuli kwenye akaunti yako, ninaweza kukupa uthibitisho wa shughuli hiyo. Wanapaswa kukuonyesha taarifa ili kuthibitisha kuwa wametupa pesa hizo, ”alisema.