Gavana Salim Mvurya aomboleza kifo cha mamake

Muhtasari

• Mama Sada Mgalla Nyawa alifariki wakati akipokea matibabu hospitalini.

• Anatarajiwa kuzikwa leo eneo la Mariakani katika kaunti ndogo ya Kinango.

Marehemu mama Sada Mgalla Nyawa, mamake Gavana wa Kwale Salim Mvurya
Marehemu mama Sada Mgalla Nyawa, mamake Gavana wa Kwale Salim Mvurya
Image: GAVANA ALI JOHO FACEBOOK

 Gavana wa Kwale Salim Mvurya anaomboleza kifo cha mama yake mzazi Sada Mgalla Nyawa.Mama Nyawa alifariki wakati akipokea matibabu hospitalini.

Kulingana na kitengo cha mawasiliano cha kaunti ya Kwale, mama Nyawa amekuwa akiugua kwa wiki tatu zilizopita na alikuwa mara kwa mara akipelekwa na kurudishwa hospitalini kwa matibabu.

Anatarajiwa kuzikwa leo eneo la Mariakani katika kaunti ndogo ya Kinango.

Naibu Rais William Ruto kupitia akaunti yake ya Twitter amemtukuza kama mwanamke mnyenyekevu, mwenye bidii, anayeogopa Mungu na anayewajibika ambaye alilea watoto vyema.

Ruto aliombea familia na wapendwa wao kuwa na nguvu wakati huu mgumu. 

Gavana wa Mombasa Hassan Joho pia alituma risala za rambi rambi kwa familia ya marehemu.

 “Nimesikitishwa sana na habari za kifo cha Mama Sada Mgala, ambaye alikuwa mama wa kaka yetu Mh. Salim Mvurya, Gavana wa Kaunti ya Kwale.

Watu wa Mombasa na mimi tunataka kuungana na familia ya Mvurya kuomboleza Mama Sada.

Tumepoteza mama na mfano wa kuigwa kwa wanawake wengi ambao walimjua.

Mungu Mwenyezi aipe familia nguvu na uvumilivu wakati huu mgumu”, Joho alisema katika Ujumbe wake.