Gadhabu kuhusu kifo cha mtoto katika seli ya polisi

Muhtasari

• Mwili wa mtoto uliondolewa na polisi na sasa umehifadhiwa katika chumba cha wafu cha Kocholia.

Pingu
Image: Radio Jambo

Mama mmoja anatafuta haki baada ya mwanawe kufariki akiwa katika kituo cha Polisi cha Malaba kaunti ya Busia.

Hali ya taharuki ilitanda mjini humo siku ya Alhamisi baada ya mtoto wa mwaka moja na mwenzi moja kuripotiwa kufariki ndani ya seli ya polisi alikokua amekesha na mamake aliyeshikwa kwa kuuza pombe haramu ya chang'aa.

Kulingana na mamake mtoto Everline Emayoto, polisi wa kituo cha Malaba walimkamata na mwanawe mchanga aliyekua mgonjwa Jumatano jioni nyumbani kwake katika kijiji cha Agong'et kwa madai ya kuuza pombe ya chang'aa, na kumzuilia kwenye seli.

Alisema juhudi zake za kuomba apelekwe katika kituo cha afya kumtafutia mwanawe matibabu ziliambulia patupu huku polisi hao wakipuuza ombi lake na kupelekea mwanawe kufariki.

Juhudi zetu za kupata kauli ya mkuu wa polisi eneo hilo hazikufua dafu.

Mwili wa mtoto uliondolewa na polisi na sasa umehifadhiwa katika chumba cha wafu cha Kocholia.