Magoha akosoa Chuo kikuu cha Nairobi kwa kuongeza karo

Muhtasari

• Magoha alitaja ada hizo kuwa haramu na kwamba taasisi hiyo ilifanya uamuzi huo bila yeye kujua.

Waziri wa elimu George Magoha
Waziri wa elimu George Magoha
Image: KWA HISANI

Waziri wa Elimu George Magoha amekosoa uongozi wa Chuo Kikuu cha Nairobi kwa kupandisha karo katika mabadiliko yaliyotangazwa mwezi Septemba.

Mwezi Septemba, chuo kikuu cha Nairobi, kiliongeza ada ya vyumba vya kulala mara saba, kutoka Shilingi 6,000 kwa mwaka hadi Shilingi 40,000, huku karo ikiongezeka kutoka Shilingi 28,000 kwa mwaka wa masomo hadi karibu Shilingi 59,000 kwa muhula.

Magoha alitaja ada hizo kuwa haramu na kwamba taasisi hiyo ilifanya uamuzi huo bila yeye kujua.

"Nitafanya nini, sina mamlaka ya kufanya lolote katika vyuo vikuu, mamlaka hayo yaliondolewa katika marekebisho ya sheria ya usimamizi wa vyuo nchini. Kama ilivyo sasa, halmashauri za vyuo vikuu zinafanya kazi bila kuhusika kwangu, ”CS alisema.

Alizungumza wakati alipofika mbele ya Kamati ya Bunge ya Kitaifa ya elimu siku ya Alhamisi.

Waziri alisema kuwa Sheria ya Vyuo Kikuu inamzuia kuchukua hatua yoyote kwa wakuu wa vyuo vikuu na uongozi wa mabaraza ambao maamuzi yao ni haramu.

“Hivi sasa nikichukua hatua kwa baraza (Chuo Kikuu cha Nairobi) watakimbia kortini; nifanye nini? ” Alisema.

Ametoa wito kwa bunge kuharakisha marekebisho ya Sheria ya vyuo vikuu ambayo ili kurudisha itarudisha mamlaka ya usimamizi wa waziri kwa taasisi za elimu ya juu.

"Nipe nguvu tena na utaona kwamba (nyongeza ya ada katika UoN) imebadilishwa kwa mara moja,”CS alisema.

Magoha na uongozi wa Chuo Kikuu cha Nairobi hawajakuwa na uhusiano mwema tangu mwaka tangu mwaka 2019.  Pande zote mara nyingi zimetofautiana hadharani kuhusu maswalaa mbali mbali ya kisera.

Mwezi  Januari 2020 waziri alibatilisha uteuzi wa Stephen Kiama kama naibu Chansela wa chuo hicho.

Walakini, usimamizi wa chuo hicho ulikwenda mahakamani na kufanikiwa kubatilisha maagizo ya Magoha.