Boniface Mwangi akaidi maagizo ya gavana Mutua licha kuandikiwa barua ya madai

Muhtasari

•Mutua alimwagiza Mwangi afute jumbe na video za uongo ambazo alichapisha mitandaoni na kuenezwa sana mitandaoni huku akisema kwamba zilikuwa za kukera.

•Gavana huyu pia alimtaka Mwangi aandike hakikisho kwamba hatadhubutu tena kuchapisha jumbe ama video za uwongo kama alizokuwa amechapisha hapo awali

•Hata hivo Mwangi hajaonekana kutishwa na maagizo ya mwanasiasa huyo kwani kufikia asubuhi ya Ijumaa video na jumbe ambazo mwanaharakati huyo alikuwa amechapisha  akimshtumu Mutua bado zipo kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Image: INSTAGRAM/ BONIFACE MWANGI

Baada ya Boniface Mwangi kuchapisha video mitandaoni akimshtumu gavana wa Machakos Alfred Mutua kwa masaibu yaliyompata, mwanasiasa huyo hatimaye alimjibu huku akimpa madai matano ambayo alitaka mwanaharakati huyo  atimize kabla ya siku ya Alhamisi kuisha.

Kupitia kwa wakili barua iliyoandikwa na wakili wake Harrison Kinyajui, Mutua alisema  kwamba madai ya Mwangi yalikuwa ya uongo na ya kumharibia jina

Mutua alimwagiza Mwangi afute jumbe na video za uongo ambazo alichapisha mitandaoni na kuenezwa sana mitandaoni huku akisema kwamba zilikuwa za kukera.

Vile vile Mutua alimtaka Mwangi aombe msamaha  kufuatia madhara ambayo madai yake yalimsababishia. Wakili Kinyajui aliagiza Mwangi aandike msamaha kwa namna ambayo itakubalika na gavana Mutua.

"Uandike msamaha kwa njia ambayo inakubalika kwetu na kupitishwa na mteja wetu.Uchapishe msamaha kwa maneno na namna iliyopitishwa na mteja wetu na kwa uzito kama uliokuwepo kwenye chapisho hizo za kukera" Kinyajui aliandika.

Mutua alimtaka  baba huyo wa watoto watatu afute video na jumbe zote alizochapisha kumhusu kwenye mitandao na tovuti mbalimbali.

Gavana huyo pia alimtaka Mwangi aandike hakikisho kwamba hatadhubutu tena kuchapisha jumbe ama video za uwongo kama alizokuwa amechapisha hapo awali

"Iwapo utakaidi masharti yaliyo kwenye barua hii ya madai, mteja wetu atachukua hatua ya kisheria. Kufuatia hayo mteja wetu atahitaji kufidiwa madhara uliyomsababishia bila kukuarifu" Barua hiyo ilisoma.

Hata hivo Mwangi hajaonekana kutishwa na maagizo ya mwanasiasa huyo kwani kufikia asubuhi ya Ijumaa video na jumbe ambazo mwanaharakati huyo alikuwa amechapisha  akimshtumu Mutua bado zipo kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Hali kadhalika hakuna hakikisho  kana kwamba mwanaharakati huyo amemwomba gavana Mutua msamaha kama alivyokuwa ameagiza.