"Upendo tu ndio tunao" Juliani azungumza baada ya nyumba ya Boniface Mwangi kushambuliwa

Muhtasari

•Juliani ambaye siku za hivi karibuni amekuwa akionekana sana na mwanaharakati huyo amesema kwamba hawana chuki kwa yeyote hata wanaowatakia mabaya.

•Mwangi alidai kwamba mwanasiasa huyo amekuwa akipatia Juliani na mpenzi wake Lilian Ng'ang'a vitisho ili wabaki kimya  ila akaeleza kuwa yeye haogopi kwani amelindwa na nguvu zake Maulana.

Image: INSTAGRAM// BONIFACE MWANGI

Masaa machacha baada ya mwanaharakati Boniface Mwangi kutangaza kwamba nyumba anayojenga katika maeneo ya Lukenya, rafiki yake mwanamuziki Julius Owino almaarufu kama Juliani amechapisha ujumbe unaoonekana kuzungumzia tukio hilo.

Juliani ambaye siku za hivi karibuni amekuwa akionekana sana na mwanaharakati huyo amesema kwamba hawana chuki kwa yeyote hata wanaowatakia mabaya.

"Mapenzi ndio tu tunayo, hata kwa wale ambao wanatutakia mabaya yatutendekee" Juliani aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Ujumbe wake unajiri masaa machache baada ya raifiki yake Boniface Mwangi kudai kuwa genge la majambazi ambalo anaamini lilitumwa na mwanasiasa ambaye ana ugomvi naye lilishambulia nyumba yake kwa bomu na risasi na kuwaibia wafanyikazi wake.

"Majambazi walivamia nyumba yangu ambayo inajengwa, wakalipua msingi wa nyumba na kuibia wafanyikazi wangu. Siwezi enda huki kwa sababu za kiusalama" Mwangi alisema.

Baba huyo wa watoto watatu alisema kwamba risasi ambazo zilitumika pamoia na vilipuzi vingali katika eneo la tukio.

Mwangi alihusisha mwanasiasa mmoja mashuhuri nchini na tukio hilo huku akitoa ombi kwa serikali kulichunguza  kwa kina .

"Risasi na vilipuzi vingali katika eneo la tukio. Kwani tunaishi katika nchi gani?.. Bado siogopi kwani Mungu ni mchungaji wangu, sitataka zaidi, atanilinda.. Kwa serikali, risasi na vilipuzi vingali kwa kiwanja changu. Ninachoomba ni muanzishe uchunguzi wa kina na wazi. Kama kuongea ukweli kutafanya niuliwe, niko tayari kufa. Naumia lakini roho yangu bado haijavunjika. Hata haya yatapita" Mwangi alisema.

Mwangi alidai kwamba mwanasiasa huyo amekuwa akipatia Juliani na mpenzi wake Lilian Ng'ang'a vitisho ili wabaki kimya  ila akaeleza kuwa yeye haogopi kwani amelindwa na nguvu zake Maulana.

Polisi wamesema kwamba wanachunguza tukio hilo ambalo liliokea usiku wa Jumatano huku mjadala mkubwa ukiendelea mitandaoni kuhusiana na suala hilo.