Echesa na OCS wa Mumias washikana matai kuhusu mrembo

Muhtasari

Wakati wa vurumai hizo, gari aina ya Mercedes-Benz inayomilikiwa na Munyendo linadaiwa kuharibiwa vibaya na OCS.

Aliyekuwa waziri wa Michezo Rashid Echesa
Aliyekuwa waziri wa Michezo Rashid Echesa
Image: MERCY MUMO

Waziri wa zamani wa Michezo, Rashid Echesa, siku ya Alhamisi akijipata katika patashika na afisa wa polisi kuhusu mwanamke katika kaunti ndogo ya Mumias Mashariki.

Kulingana na ripoti ya polisi, Echesa alihusika katika rabsha na afisa wa polisi wa cheo cha OCS katika Klabu cha usiku cha Jose Lounge and Grill mjini Mumias ikihusisha.

Iliripotiwa na mtu kwa jina Rajab Munyendo kwamba wakati walikuwa wakinywa pombe, mwanamume mmoja aligusa visivyo mwanamke ambaye alikuwa ameandamana na OCS.

Kitendo hiki kilisababisha ugomvi kati ya vikundi hivyo viwili.

Wakati wa vurumai hizo, gari aina ya Mercedes-Benz inayomilikiwa na Munyendo linadaiwa kuharibiwa vibaya na OCS.

Munyendo pia anadai kwamba alipoteza Shilingi 77,000 wakati wa kisa hicho.

Polisi wanachunguza kisa hicho.

Echesa anakabiliwa na kesi nyingine ya kupanga njama kufanya uhalifu.

Anatuhumiwa kula njama kutengeneza hati kwa nia ya kulaghai katika sakata ya makubaliano bandia ya ununuzi wa silaha mabilioni.

Waziri huyo wa zamani ameshtakiwa pamoja na Daniel Omondi aliyejulikana kwa jina Jenerali Juma, Clifford Onyango, Chrispine Oduor na Kennedy Mboya na makosa sita ya kutengeneza hati ya uwongo.

Wanadaiwa pia kupata Shilingi milioni 11.5 milioni kutoka kwa Kozlowski Stanley Bruno kwa kudai kwamba watampa zabuni ya kusambaza vifaa vya kijeshi.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO