Jamaa wawili wakamatwa baada ya 'lori la saruji' kupatikana likiwa limebeba mifuko 89 ya bangi, Thika

Muhtasari

•Hassan Adan Maalim 25, na Shedrack Maangi  35, walikamatwa na wapelelezi wa DCI baada ya kubainika kwamba lori lililokuwa limebandikwa jina 'Rhino Cement' ambalo walikuwa nalo halikuwa limebeba saruji ila lilikuwa linasafirisha bangi.

Image: TWITTER// DCI

Wapelelezi wa DCI wanazuilia washukiwa wawili wa biashara ya madawa ya kulevya baada ya lori ambalo walikuwa nalo kunaswa na mifuko 89 ya bangi.

Hassan Adan Maalim 25, na Shedrack Maangi  35, walikamatwa na wapelelezi wa DCI baada ya kubainika kwamba lori lililokuwa limebandikwa jina 'Rhino Cement' ambalo walikuwa nalo halikuwa limebeba saruji ila lilikuwa linasafirisha bangi.

Wapelelezi wa DCI walikuwa wamepokea ripoti kuhusu genge la wahalifu ambalo lilikuwa linaendeleza biashara la ya madawa ya kulevya wakijifanya kuwa wafanyikazi huku wakitumia  magari ambayo yamebandikwa majina ya makampuni makubwa.

Lori hilo nambari KBS 601M lilinaswa katika barabara ya Garissa Road likiwa linasafirisha vifurushi  hivyo kutoka Wajir kuelekea Nairobi.

Washukiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani siku ya Jumatatu. Lori hilo pamoja na mifuko ya bangi iliyopatikana zitatumika kama ushahidi mahakamani.