Polisi aliyeua mwenzake kwa kumtusi 'kihii' ahukumiwa kifungo cha miaka 40

Mshtakiwa alisema kwamba matendo yake yalisababishwa na uchokozi wa marehemu

Muhtasari

•David Muriuki alihukumiwa kifungo hicho baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kwamba alitekeleza mauaji ya Joseph Mwita katika kituo cha polisi cha Witu, kaunti ya Lamu mnamo mwaka wa 2015.

•Mshtakiwa alisema kuwa alipouliza marehemu sababu za kumtusi alisema kuwa aligongwa na chupa ya pombe kichwani.

Mahakama
Mahakama

Polisi ambaye alipiga afisa mwenzake risasi katika kituo cha polisi kufuatia mzozo uliotokea baada ya kutusiwa kuwa hajatahiri amehukumiwa kifungo cha miaka 40.

David Muriuki alihukumiwa kifungo hicho baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kwamba alitekeleza mauaji ya Joseph Mwita katika kituo cha polisi cha Witu, kaunti ya Lamu mnamo mwaka wa 2015.

Mnamo Oktoba 28 , Jaji Reuben Nyakundi aliamuru kuwa mahakama ilikuwa imempata mfungwa na hatia ya mauaji na kumhukumu kifungo cha miongo minne gerezani.

Masudu Sabur alitoa ushahidi kuwa mnamo Mei 21, 2015 alikuwa anafanya kazi ya kutunza bustani katika kituo cha polisi cha Witu. Siku hiyo alikuwa na mshtakiwa katika duka la polisi kisha baadae marehemu akaungana nao.

Alisema kwamba mshtakiwa ambaye kwa wakati huo alikuwa amejihami na bunduki aliagiza afisa marehemu asimame ila akaendelea na safari na kuelekea kwenye eneo la kupokea wageni ambapo aliangalia kitabu cha OB.

Shahidi alisema kwamba alisikia milio ya risasi ambazo zililenga marehemu. Alisema kuwa alimuona marehemu akiwa amepoteza fahamu huku akitokwa na damu kwenye tumbo . Kwa wakati huo Muriuki alikuwa ameshika bunduki.

Esau Baraza alisema kwamba siku ile alikuwa ametembelea baba yake pale katika kituo cha Witu. 

Alisema kuwa mshtakiwa aliagiza bia ya Tusker na kabla hajamaliza kuibugia, marehemu akaingia kwenye duka.

Alisema kwamba alisikia mshtakiwa akimuita marehemu mara tatu lakini hakusikia majibu. Marehemu alienda kama ameingia kwenye chumba cha kupokea wageni. Mshtakiwa akamfuata hadi pale na Baraza akasikia milio ya risasi.

Sajenti Stephen Melia ambaye alifanya kazi katika kituo hicho alisema kwamba siku hiyo alimuacha marehemu katika ofisi ya kupigia ripoti.

Alipofika kwenye lango alimuona mshtakiwa akiwa anatoroka huku akiwa amebeba bunduki. Alikuwa amefuatwa nyuma na mtu mwingine ambaye alikuwa anamwagiza asimame ili aeleze mbona alikuwa ameua mtu.

Afisa huyo alisema kuwa alimkamata mshtakiwa, akachukua bunduki yake na kumpeleka katika ofisi ya kupigia ripoti.

Patrick Kimathi ambaye ni mfanyibiashara katika eneo la Witu alisema kwamba alikuwa katika baa yake iliyo katika kituo cha Witu wakati ambapo alishuhudia mabishano kati ya mshtakiwa na marehemu.

Wakati mabishano yalikuwa yamechacha alielekea hadi walipokuwa wamekaa na kuuliza kilichokuwa kimesababisha kutoelewana kule.

Wakati huo alimsikia mshtakiwa akimuita marehemu 'Kihii' kumaanisha mwanaume ambaye hajatahiriwa.

Kwa hasira marehemu akamwagia mshtakiwa pombe kichwani na hapo wakaanza kuvurugana kabla ya maafisa wengine kufika na kusitisha vita ile.

Mshtakiwa alipata jeraha wakati wa vita ile. Wote wawili walitoka pale kwenye baa baada ya vita kusitishwa.

Alipokuwa anajitetea, Muriuki alisema kuwa kulikuwa na mabishano kati yake na mwenzake ambaye alitambulisha kama Ndwegwa katika eneo moja la umma.

Alisema kuwa aliagiza bia na viazi na marehemu akauliza mbona sahani yake ilionekana tofauti na ile aliyopata.

Alisema kuwa marehemu alimuita 'kihii', mtu ambaye hajatahiriwa.

Mshtakiwa alisema kuwa alipouliza marehemu sababu za kumtusi alisema kuwa aligongwa na chupa ya pombe kichwani.

Mshtakiwa aliambia mahakama kwamba aliondoka pale kwenye klabu na kuelekea kwa duka . Alisema kwamba marehemu alimfuata nyuma na mzozo ukaendelea kuchacha.

Mshtakiwa alisema kwamba matendo yake yalisababishwa na uchokozi wa marehemu.

(Utafsiri: Samuel Maina)