Mwanamke akiri kujiunga na Al-Shabaab baada ya kutekwa nyara na kupelekwa Somalia miaka 2 iliyopita

Muhtasari

•Mwanadada huyo alipotiwa mbaroni alikiri kuwa mwanachama wa kundi hilo haramu huku akidai alilazimishwa  kujiunga nao baada ya kutekwa nyara miaka miwili iliyopita.

•Alikiri kupatiwa mafunzo ya wanamgambo alipokuwa Somalia ikiwemo kutumia silaha, kuteka watu nyara, kutumia vilipuzi ikiwemo mafunzo mengine.

Pingu
Pingu Pingu
Image: Radio Jambo

Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 22 alikamatwa jioni ya Jumanne katika eneo la Tinderet, kaunti ya Nandi baada ya kuhusishwa na kikundi cha kigaidi cha Al Shabab.

Kulingana na DCI, mwanamke huyo alikamatwa baada ya wanakijiji wa Kamalambu kupiga ripoti kuhusu mwanamke aliyetiliwa shaka ambaye alikuwa anaishi na mwanaume.

Mwanadada huyo alipotiwa mbaroni alikiri kuwa mwanachama wa kundi hilo haramu huku akidai alilazimishwa  kujiunga nao baada ya kutekwa nyara miaka miwili iliyopita.

Alieleza polisi kwamba alitekwa nyara na wanamgambo wa Al Shabab katika kaunti ya Kilifi mnamo mwaka wa 2019 na kupelekwa hadi nchi jirani ya Somalia.

Mwanadada huyo alikiri kupatiwa mafunzo ya wanamgambo alipokuwa Somalia ikiwemo kutumia silaha, kuteka watu nyara, kutumia vilipuzi ikiwemo mafunzo mengine.

Inaripotiwa mwanamke huyo alijitokeza katika majaribio ya kusajili wanajeshi wa KDF ambayo ilitamatika hivi majuzi.

Maafisa wa kupambana na ugaidi wanaendeleza uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo ikiwemo kumhoji zaidi mshukiwa huyo.