Hakuna mabadiliko yoyote katika tarehe za mitihani ya KCPE na KCSE- KNEC

Muhtasari

• KNEC imesema habari zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuahirishwa kwa mitihani ya mwaka ujao si za kweli.

Watahiniwa wa darasa la nane wakalia mtihani wa KCPE
Watahiniwa wa darasa la nane wakalia mtihani wa KCPE
Image: MAKTABA

Baraza la mitihani la Kenya (KNEC) limepuuzilia mbali madai ya kuahirishwa kwa mitihani ya kitaifa ya darasa la nane (KCPE) na kidato cha nne (KCSE).

Kupitia kwa taarifa iliyotolewa na mkurugenzi mtendaji David Njengere siku ya Alhamisi, KNEC ilisema habari zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuahirishwa kwa mitihani ya mwaka ujao si za kweli.

KNEC imesema hakuna mabadiliko yoyote ambayo yamefanywa katika tarehe za mitihani ya kitaifa ya KCSE na KCPE.

"Tunataka kuwafahamisha washikadau wote husika kwamba hakuna mabadiliko yoyote katika tarehe za mitihani ya kitaifa ya KCPE na KCSE" KNEC ilisema.

Watahiniwa wa KCPE 2021/22wanatarajiwa kuanza mtihani wao mnamo Machi 7, 2022 na kutamatika tarehe Machi 9.

Mtihani wa KCSE 2021/22  utang'oa nanga mnamo Februari 22, 2022 na kuendelea hadi tarehe mosi mwezi Aprili, 2022.