Wakenya 4,579 walifariki, 16, 046 walijeruhiwa katika ajali za barabarani mwaka jana- Oguna asema

Muhtasari

•Oguna amelaani uendeshaji wa magari kwa mwendo wa kasi huku akiutaja kama kiini kikuu cha ajali za barabarani.

•Madereva wa magari ya umma na ya kibinafsi wameagizwa kuwa makini zaidi na kutii sheria zote za barabarani ili kuzuia kupatikana kwa ajali zaidi.

Msemaji wa Serikali Cyrus Oguna
Msemaji wa Serikali Cyrus Oguna
Image: MAKTABA

Mwaka uliopita Wakenya 4, 579 walipoteza maisha yao na wengine 16, 046 kujeruhiwa katika ajali za barabarani, msemaji wa serikali Cyrus Oguna amesema.

Katika taarifa yake kuhusu usalama barabarani huku shule zikifunguliwa, Oguna alisema wanafunzi waliokuwa wanaelekea nyumbani baada ya shule kufungwa ni miongoni mwa waliopoteza maisha yao katika ajali hizo.

Oguna amelaani uendeshaji wa magari kwa mwendo wa kasi huku akiutaja kama kiini kikuu cha ajali za barabarani.

"Kufikia mwishoni mwa mwaka jana (2021), nchi ilikuwa imepoteza watu 4,579 katika ajali za barabarani ambazo zingeweza kuepukika. Watu 16,046 waliuguza majeraha. Baadhi ya walioangamia ni wanafunzi waliokuwa wakirejea nyumbani. Mwendo kasi umekuwa chanzo kikuu cha ajali hizo. Hili halikubaliki, na sisi (kwa pamoja), lazima tukomeshe" Oguna alisema.

Msemaji huyo wa serikali amesema familia nyingi zinapoteza tegemeo lao na watoto wengi kuachwa mayatima kufuatia ajali za barabarani.

Kufuatia hayo madereva wa magari ya umma na ya kibinafsi wameagizwa kuwa makini zaidi na kutii sheria zote za barabarani ili kuzuia kupatikana kwa ajali zaidi.

"Endesha kwa kuwajibika, na tuwafikishe watoto wetu wote shuleni kwa usalama. Wasafiri wote, ikiwa ni pamoja na wanafunzi wanaorejea shuleni, wanahimizwa kuzungumza dhidi ya uendeshaji mbaya wa magari. Kumbuka, uhai wako ni zawadi yenye thamani kutoka kwa Mungu. Usimwamini dereva yeyote nayo! Usalama barabarani lazima uwe wa wasiwasi kwetu sote" Amesema Oguna.