Moses Kuria akana ripoti kuwa anatazamia kuwania kiti cha ugavana Kiambu

Muhtasari

•Hii ni baada ya bango lililoundwa vizuri kuibuka likidai kwamba anamezea mate kiti hicho na kuwa mjumbe wa wadi ya Biashara katika kaunti hiyo Elijah Njoroge atakuwa mgombea mwenza wake.

•Kuria amekanusha, na kuongeza kuwa yeye huwasiliana tu kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Mbunge wa Gatunndu Kusini, Moses Kuria
Moses Kuria Mbunge wa Gatunndu Kusini, Moses Kuria
Image: Courtesy

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria amekanusha vikali madai kwamba anavutiwa na kiti cha ugavana wa Kiambu ambacho kinatamaniwa sana.

Hii ni baada ya bango lililoundwa vizuri kuibuka likidai kwamba anamezea mate kiti hicho na kuwa mjumbe wa wadi ya Biashara katika kaunti hiyo Elijah Njoroge atakuwa mgombea mwenza wake.

Bango hilo lilikuwa likisambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Hapo awali Njoroge alikuwa ameonyesha kuvutiwa na wadhifa wa Seneta wa Kaunti ya Kiambu.

Alipoulizwa kuhusu uhalisi wa bango hilo, MCA huyo alikubali lakini hakuweza kufikiwa kwa habari zaidi.

Lakini Kuria amekanusha, na kuongeza kuwa yeye huwasiliana tu kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

"Ninafanya matangazo yangu kwenye ukurasa wangu," Kuria amesema.

Mbunge huyo yuko nje ya nchi akitafuta matibabu zaidi baada ya kuugua takriban miezi michache iliyopita. Amefanyiwa upasuaji mara kadhaa.

Mbunge huyo alijeruhiwa baada ya kutumia mkeka wa umeme ili kutibu ganzi katika miguu yake.

Ikiwa kiongozi huyo wa Chama Cha Kazi angejipa uzito katika kinyang'anyiro cha Ugavana wa Kiambu, angechuana vikali na gavana James Nyoro, aliyekuwa Gavana William Kabogo, Seneta Kimani Wamatangi, Mbunge wa Thika Patrick Wainaina (Wajungle), aliyekuwa gavana Ferdinand Waititu na Spika wa Bunge la Kaunti ya Kiambu Stephen Ndicho.

Chama cha Kuria kimekuwa kikishika kasi katika eneo la Kati mwa Kenya, huku wagombeaji wengi wakionyesha nia ya kuwania nyadhifa mbalimbali kwa tiketi ya CCK.

(Utafsiri: Samuel Maina)