Mwanadada aliyeuawa na mwili wake kuwekwa kwenye mkoba atambulishwa

Muhtasari

•Siku alipofariki, mpenzi wake alikuwa amemsindikiza hadi kwenye makutano yaliyo takriban kilomita moja kutoka eneo lake la kazi.

•Maafisa wa upelelezi wanaoshughulikia kesi hiyo walisema wanashuku mwanamke huyo alishambuliwa na wauaji, ambao pengine walimbaka kisha kuamua kumuua.

crime scene
crime scene
Image: MAKTABA

Mwanamke ambaye mwili wake ulipatikana ukiwa umewekwa kwenye kijisanduku katika maeneo ya Ruiru ametambuliwa.

Polisi wamesema familia yake imethibitisha kuwa mwanamke huyo ni Esther Wambui, 18, ambaye alifanya kazi katika hoteli moja iliyo eneo hilo kama mhudumu.

Aliviziwa na kuuawa na watu wasiojulikana alipokuwa anaelekea kazini mnamo Januari 17 asubuhi.

Kulingana na uchunguzi wa awali, mwanamke huyo alikuwa amefanya kazi kwenye mkahawa huo kwa kipindi cha chini ya wiki mbili.

Siku alipofariki, mpenzi wake alikuwa amemsindikiza hadi kwenye makutano yaliyo takriban kilomita moja kutoka eneo lake la kazi.

Joseph Ngige aliwaambia polisi kuwa huwa anafanya kazi katika kituo cha mafuta kilicho eneo hilo. Alisema alikuwa amemsindikiza na kumwaga mpenzi wake akitarajia kumuona jioni kama kawaida.

Ngige aliwaambia polisi kuwa hafahamu ni kwa nini mpenzi wake aliuawa kikatili na mwili wake kuwekwa  kwenye kijisanduku. Alisema Wambui hakuwa na simu.

Wote wawili wanatoka Nakuru na waliishi katika nyumba moja katika mtaa wa Ruiru.

Polisi walisema familia ya marehemu ilikwenda katika kituo cha polisi cha Juja na baadaye kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti, ambapo walifanikiwa kuutambua mwili huo.

Maafisa wa upelelezi wanaoshughulikia kesi hiyo walisema wanashuku mwanamke huyo alishambuliwa na wauaji, ambao pengine walimbaka kisha kuamua kumuua.

Tunaamini kuwa ujumbe ulioandikwa kwenye mwili wake ulikuwa na lengo la kupotosha uchunguzi,” alisema afisa anayefahamu kuhusu kisa hicho.

 Mwili huo ulipatikana Jumatatu jioni ukiwa umetupwa nje ya kambi ya kikosi cha Recce cha GSU kilicho maeneo ya Ruiru, Kaunti ya Kiambu. 

Timu ya wapelelezi kutoka Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai kutoka Ruiru wametembelea nyumba aliyokuwa akiishi mwanamke huyo na eneo ambalo mwili huo ulipatikana. 

Polisi walisema mwanamke huyo alikatwakatwa hadi kufa.  

Mwili ulikuwa umekatwakatwa na kufichwa kwenye sanduku huku mikono yake ikiwa imefungwa kwa nyuma.  

Mwili huo ulikuwa na ujumbe uliodhaniwa kuwa kutoka kwa wauaji ambao ulisoma "Bwana ya mtu ni sumu". 

Ujumbe huo ulikuwa umeandikwa kifuani, kwenye viganja vyake na mapajani.

 Mwili huo ulikuwa umewekwa kwenye gunia ya nailoni kabla ya kuwekwa kwenye kijisanduku. Sababu ya mauaji hayo bado haijajulikana, polisi walisema.

Kwa mujibu wa polisi na mashahidi, miguu ilikuwa imefungwa kwa kamba na mikono ilikuwa imefungwa nyuma.Titi lake la kushoto lilikuwa limekatwa na shingo yake ilikuwa na kamba ya nailoni. 

Mkuu wa DCI  katika eneo la Ruiru Justus Ombati alisema mwanamke huyo huenda aliuawa kwingine na kutupwa kando ya ukuta wa kituo chenye ulinzi mkali cha GSU Recce. 

Matukio kama haya ni ya kawaida katika mkoa huo. Baadhi zimeunganishwa na pembetatu ya upendo, na zingine na mali.Polisi wanasema wamesuluhisha zingine huku zingine zikiwa hazijatatuliwa.

(Utafsiri: Samuel Maina)