Mike Sonko afunguka kuhusu wakati alikusudia kujitoa uhai ndani ya City Hall

Muhtasari

•Sonko amesema tatizo la msongo wa mawazo ni la kawaida haswa miongoni mwa wanaume na aghalabu huwa hawapati usaidizi kwa muda ufaao.

•Amesema marafiki wake walimshauri aanze vita na mdosi wake ambaye kisha baadae wakawa vigeugeu na kuenda kwa mdosi huyo kumchochea wakitaka atimuliwe.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Image: HISANI

Siku ya Alhamisi Kenya iliamkia habari za kuhuzunisha kuhusu kifo cha DJ maarufu ambaye anaripotiwa kujitoa uhai katika ofisi za kituo kimoja cha redio cha hapa nchini.

DJ Lithium aliripotiwa kufariki katika hospitali ya Nairobi alipokuwa anapokea matibabu baada ya kuzimia mbele ya wafanyikazi wenzake.

Wanamitandao wameendelea kumwomboleza mcheza santuri huyo huku wakitoa hisia mbalimbali kufuatia kisa hicho cha kusikitisha.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko amesema tatizo la msongo wa mawazo ni la kawaida haswa miongoni mwa wanaume na aghalabu huwa hawapati usaidizi kwa muda ufaao kwani wengi wao hupendelea kusalia kimya na kupambana na hali yao kivyao.

"DJ Lithium ajitoa uhai katika ofisi za redio. Aki sisi Wanaume wakati mwingine huwa tunapitia msongo wa mawazo na huwa hatufungukii marafiki kama jinsi wanawake wanavyojadili mambo yao na wanawake wenzao juu asilimia 90 ya maadui wetu ni marafiki wetu" Sonko amesema.

Mwanasiasa huyo pia ametumia fursa hiyo kufunguka kuhusu wakati fulani alipokuwa gavana bado ambapo alipatwa na mawazo ya kujitoa uhai baada ya kupewa ushauri potovu na rafiki yake.

Sonko amesema marafiki wake walimshauri aanze vita na mdosi wake ambaye hajatambulisha jina kisha baadae wakawa vigeugeu na kuenda kwa mdosi huyo kumchochea dhidi yake wakitaka atimuliwe.

"Kuna wakati nilikaribia kujitoa uhai pale City Hall baada ya kugundua marafiki zangu wa karibu kwenye baraza la kaunti na mmoja kutoka EALA walinichochea na kunishauri nianze vita na beste yangu fulani baada ya kutambua kuna Jeshi aliletwa kuendeleza NMS na walipoona anaendea na pesa nyingi huko. Tulipo kaa chini kama mabeste kujadili wakanichocha ati huyu mdosi sasa ametuzoea hebu mvuruge live live na ana kwa ana na baada ya hapo  akaenda kwa  mdosi huyo huyo tu na kumwambia ona vile Sonko anakuvuruga afadhali huyu mtu tumtoe" Sonko amesimulia.

Gavana huyo wa zamani amesema tukio hilo lilimfunza kwamba kikulacho kweli ki nguoni.

Amewashauri Wakenya kutahadhari dhidi ya marafiki ambao hujifanya waaminifu ila hawana nia njema dhidi yao.