Magix Enga akusudia kufungua kanisa baada ya kugura Illuminati

Muhtasari

•Msanii huyo  ameweka wazi kwamba kwa sasa hayuko tena Illuminati na kudai kuwa tayari amemkubali yesu maishani mwake na kuokoka.

•Alisema atatumia kanisa lake kuelimisha watu kuhusu madhebehu ya kishetani na kuwatahadharisha dhidi ya kujiunga nayo.

Image: FACEBOOK// MAGIX ENGA

Baada ya kufichua kwamba aliwahi kuwa mwanachama wa Illuminati, mwanamuziki na mzalishaji tajika Magix Enga sasa anadai kwamba anakusudia kufungua kanisa.

Akiwa kwenye mahojiano na Plug TV, Magix Enga alisema sababu yake kuu ya kutaka kufungua kanisa ni kwa kuwa  angependa kusaidia wengine ambao wanapitia masaibu kama aliyopitia baada ya kugura Illuminati na kuwonyesha mwelekeo mzuri wa maisha.

Msanii huyo  ameweka wazi kwamba kwa sasa hayuko tena Illuminati na kudai kuwa tayari amemkubali yesu maishani mwake na kuokoka.

"Saa hii mimi nimeokoka sana. Hata napanga kufungua kanisa ili nizidi kusaidia wasee wanapitia  mambo kama  ile napitia na kuwaonyesha mwelekeo wa kuwa waumini. Ata kama sitakuwa mhubiri, nitakuwa na kanisa," Magix Enga alisema.

Mtayarishaji huyo wa muziki alisema atatumia kanisa lake kuelimisha watu kuhusu madhebehu ya kishetani na kuwatahadharisha dhidi ya kujiunga nayo.

Magix pia alifichua kwamba kuna Wakenya wengi haswa wasanii ambao ni wanachama wa makundi hayo.

"Ajenda kuu itakuwa kuambia watu ukweli kuhusu upande wa giza wa dunia hii kwa sababu hawaujui. Wasanii ni wengi lakini siwezi wataja kwa kuwa sitaki kujiweka kwa shida  siwezi kujitoa, ndio maana nimesema mimi pekee yangu, sitaki kumwingiza mwingine kwa stori hii," Magix alisema.

Hivi majuzi msanii huyo alifichua kwamba alijiunga na Illuminati akiwa na umri wa miaka 23. Alisema alijipatia utajiri mkubwa kutokana na kujiunga na kikundi hicho.