Sitajiuzulu! Waziri Munya asema hatawania ugavana Meru

Muhtasari

• Waziri wa kilimo, Peter Munya amesema kwamba hatojiuzulu ili kuwania kiti cha ugavana kaunti ya Meru.

• Munya amesema kwamba lengo lake kwa sasa ni kumsaidia rais Uhuru Kenyatta kutimiza malengo yake katika ruwaza yake ya ajenda nne kuu.

Munya
Munya

Waziri wa kilimo, Peter Munya amesema kwamba hatojiuzulu ili kuwania kiti cha ugavana katika kaunti ya Meru.

Kwa muda mrefu sasa, Munya alikuwa amekisiwa kwamba angeingia debeni ili kuchukua nafasi ya gavana wa sasa Kiraitu Murungi.

Munya amesema kwamba atasalia ofisini hadi wakati rasmi ambapo serikali ya Jubilee itamaliza kipindi chake cha uongozi.

Akizungumza wakati ambapo katibu wa kudumu katika wizara ya kilimo, Hamadi Boga alikuwa akijiuzulu ili kujitosa katika kinyang’anyiro cha ugavana kaunti ya Kwale, Munya amesema kwamba lengo lake kwa sasa ni kumsaidia rais Uhuru Kenyatta kutimiza malengo yake katika ruwaza yake ya ajenda nne kuu.

Waziri huyo ambaye ameonekana kuegemea upande wa mrengo wa Azimio la Umoja alikuwa gavana wa kwanza wa Meru huku wengi wakitarajia kwamba angekuwa debeni katika uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti mwaka huu.

Kimunya hata hivyo aliahidi kunadi sera za na kupigia debe muungano wa Azimio ili kunyakuwa urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Munya
Munya