Mwanaharakati Boniface Mwangi hatarini ya kufungwa jela

Muhtasari

•Mwangi alikuwa ameagizwa kujifikisha mahakamani mwenyewe kueleza sababu kwa nini asifungwe kwa kukaidi maagizo ya mahakama.

•Wakili wa Mwangi alikuwepo lakini sheria inadai kwamba katika kesi za kudharau mahakama, mshtakiwa anafaa kufika mwenyewe

Mwanaharakati Boniface Mwangi
Mwanaharakati Boniface Mwangi
Image: HISANI

Mwanaharakati Boniface Mwangi yuko hatarini ya kufungwa jela kwa kudharau mahakama baada ya kukosa kueleza sababu za kutohudhuria kesi inayomkabili ya kumharibia jina Gavana wa Machakos Alfred Mutua.

Jaji George Odunga alimwita Mwangi mahakamani kwa mara ya pili na anamtaka ajifikishe mwenyewe  hivi karibuni.

Mahakama inatarajiwa kutoa uamuzi mnamo Februari 22, 2022.

Mwanaharakati huyo alikuwa ameagizwa kujifikisha mahakamani mwenyewe kueleza sababu kwa nini asifungwe kwa kukaidi maagizo ya mahakama.

Gavana Mutua aliwasilisha kesi ya dharau ya mahakama dhidi ya Mwangi akimtaja kama mwenye mazoea ya kukaidi maagizo ya mahakama katika kesi inayowahusu.

Kupitia kwa wakili Harrison Kinyanjui, Mutua anamtaka mwanaharakati huyo aeleze sababu kwa nini hapaswi kuzuiliwa kwa kudharau mahakama kwa kukiuka agizo lililomkataza kuchapisha machapisho ya kumharibia jina.

"Mwangi alikaidi agizo hilo mnamo tarehe 6 na 9 Januari 2022 kwa kuchapisha machapisho dhidi ya Mutua kwenye akaunti yake ya Twitter," Kinyajui alisema

Wakili wa Mwangi alikuwepo lakini sheria inadai kwamba katika kesi za kudharau mahakama, mshtakiwa anafaa kufika mwenyewe.