Moses Kuria akataa Azimio, atoa masharti ya kujiunga na OKA

Muhtasari

•Kuria aliweka wazi kuwa yuko tayari kujiunga na muungano huo kwa masharti kwamba hawatajiunga na Azimio.

•Hali hii inazua shaka katika hatua ya Kalonzo kujiunga na Azimio baada yake kuonyesha nia yake siku ya Ijumaa.

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria katika mkutano na viongozi wa OKA Jumapili, Februari 26,2022.
Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria katika mkutano na viongozi wa OKA Jumapili, Februari 26,2022.
Image: FACEBOOK// MOSES KURIA

Kiongozi wa Chama Cha Kazi (CCK) Moses Kuria ameonyesha nia yake ya kufanya kazi na Muungano wa One Kenya Alliance. (OKA)

Siku ya Jumapili mbunge huyo wa Gatundu alikutana na viongozi wa muungano huo wakiwemo Kalonzo Musyoka (Wiper), Martha Karua (Narc Kenya), Cyrus Jirongo (UDP) na George Wainaina ambaye aliwakilisha Gideon Moi wa KANU.

Akizungumza baada ya kukutana na viongozi hao, Kuria alisema kuwa chama chake cha CCK kilipokea mwaliko wa kujiunga na OKA.

Mgombeaji huyo wa ugavana wa Kiambu aliweka wazi kuwa yuko tayari kujiunga na muungano huo kwa masharti kwamba hawatajiunga na Azimio.Kuria alisema muungano wa Azimio hauendani naye wala chama chake.

Walinialika mimi na Chama Cha Kazi ili tujiunge na Muungano wa One Kenya. Ingawa kuna mawazo mengi yanayowiana kati ya Chama Cha Kazi na OKA, tulikubaliana kufanya kazi pamoja mradi OKA isijiunge na Muungano wa Azimio ambao hauendani na mimi na Chama Cha Kazi," Kuria alisema.

Mbunge huyo alitangaza kuwa atashiriki kikao kingine na viongozi hao wa OKA siku ya Jumatano  ili kujua hatima ya mpango huo.

Hali hii inazua shaka katika hatua ya Kalonzo kujiunga na Azimio baada yake kuonyesha nia yake siku ya Ijumaa.