DP Ruto aondoka nchini kwa ziara ya siku 12 Marekani na Uingereza

Muhtasari

•Anatarajiwa kuchukua mapumziko ya siku 12 kutoka kwa kampeni za kisiasa zinazoendelea kuchacha ili kushughulikia masuala mbalimbali katika mataifa hayo mawili.

•Ababu alisema ziara ya Ruto inalenga kuimarisha zaidi uhusiano kati ya Kenya na marafiki wake na washirika wa jadi.

Naibu Rais William Ruto, mkuu wa sekretarieti yake ya kampeni Gavana Josephat Nanok na Gavana wa Kwale Salim Mvurya katika JKIA Jumapili, Februari 26.
Naibu Rais William Ruto, mkuu wa sekretarieti yake ya kampeni Gavana Josephat Nanok na Gavana wa Kwale Salim Mvurya katika JKIA Jumapili, Februari 26.
Image: DPPS

Naibu Rais William Samoei Ruto anaondoka nchini asubuhi ya Jumapili kwa ziara ya wiki mbili Uingereza na Marekani.

Ruto anatarajiwa kuchukua mapumziko ya siku 12 kutoka kwa kampeni za kisiasa zinazoendelea kuchacha ili kushughulikia masuala mbalimbali katika mataifa hayo mawili. 

Mkuu wa sekretarieti ya kampeni zake za urais, Gavana Josephat Nanok alimzidikisha  hadi  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.

Gavana wa Kwale Salim Mvurya pia alikuwepo.

Hapo awali mkuu wake wa uhusiano wa Kimataifa Ababu Namwamba alikuwa ametangaza kuhusu ziara hiyo. 

Namwamba alisema naibu rais alikuwa amealikwa na maafisa wakuu na taasisi kadhaa za juu za sera jijini Washington, DC, na London.

"Katika Washington, DC, Naibu Rais amepangwa kukutana, miongoni mwa wengine, maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Pentagon pamoja na Mshauri wa Baraza la Usalama la Kitaifa la Serikali ya Marekani (BMT)." Namwamba alisema.

Ruto atatoa mawazo yake kuhusu sera za kigeni, demokrasia, na utawala, na kueleza maono yake ya kiuchumi kwa Kenya na Afrika.

Pia atazungumza katika Ukumbi wa Carnegie kwa Amani ya Kimataifa, Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa, na katika Kituo cha Ujasiriamali cha Chuo Kikuu cha Arizona.

Ziara ya Marekani itahitimishwa kwa naibu rais kukutana na Wakenya walioko ughaibuni.

"Huko London, Ruto atakutana na maafisa wakuu wa Serikali ya Uingereza, atatembelea Kituo cha Kitaifa cha Kukabiliana na Ugaidi na kuzungumza katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola na Taasisi ya Kifalme ya Masuala ya Kimataifa (Chatham House).

Pia atazungumza na Wanadiaspora wa Kenya nchini Uingereza, na kutembelea askofu mkuu wa Canterbury, Justin Welby," Ababu aliongeza.

Ababu alisema ziara ya Ruto inalenga kuimarisha zaidi uhusiano kati ya Kenya na marafiki wake na washirika wa jadi.