Bodaboda 16 wafikishwa mahakamani kwa kumdhulumu mwanamke

Muhtasari

• Wahudumu 16  wa bodaboda ambao wanashukiwa kwa kumdhulumu mwanamke kwenye  barabara ya Wangari Maathai watasalia korokoroni hadi Alhamisi wakati mahakama itakapotoa uamuzi kuhusu ombi la polisi kuwazuilia kwa siku 20.

• Maafisa wa polisi wanataka mahakama iwazuilie 16 hao kwa siku 20 ili kuwawezesha kukamilisha uchunguzi wao.

Wahudumu 16  wa bodaboda ambao wanashukiwa kwa kumdhulumu mwanamke kwenye  barabara ya Wangari Maathai watasalia korokoroni hadi Alhamisi wakati mahakama itakapotoa uamuzi kuhusu ombi la polisi kuwazuilia kwa siku 20.

 Hakimu mkuu Robert Shikwe alisema kwamba alihitaji muda zaidi ili kutoa uamuzi dhidi ya James Mutinda, Samuel Wafula, Charles Omondi, Japhet Bosire, Hassan Farah, Wanjiku Lincon, Harrison Maina miongoni mwa wengine ambao wanashukiwa kumshambulia mwanamke tarehe 4/3/2022.

Washukiwa hao walifika mbele ya mahakama ya Milimani siku ya Jumatano wakitarajiwa kujibu mashtaka ya kumdhalilisha mwanamke baada ya kudaiwa kugongana na mhudumu wa bodaboda, kitendo ambacho kimekashifiwa vikali na Wakenya akiwemo rais Uhuru Kenyatta.

Upande wa mashtaka ulitaka mahakama iwazuilie 16 hao kwa siku 20 ili kuwawezesha kukamilisha uchunguzi wao.

 

Katika ombi lao, upande wa mashtaka ulitaka  kupata picha za CCTV za eneo la Barabara tano kwa uchunguzi zaidi.

Aidha upande wa mashtaka ulisema kwamba mwanamke huyo anatarajiwa kujaza fomu ya P3, huku akiendelea kupokea ushauri nasaha.

Kitendo hicho kiliwaghadhabisha wengi, huku rais Kenyatta akitoa amri ya waendesha bodaboda wote kusajiliwa upya katika lengo la kulainisha sekta hiyo.

Waziri wa usalama wa ndani, Fred Matiang'i alisema kwamba wizara yake inafanya kila juhudi kuhakikisha washukiwa wanakamatwa na kuchukuliwa hatua Kali za kisheria ili kuzuia kisa Kama hicho kutokea tena.

Polisi wameanzisha msako mkali kumtafuta mshukiwa mmoja zaidi Zachariah Nyaora Obadia ambaye alionekana kwa video akimshika visivyo mwanamke aliyekuwa akidhulumiwa.