Raila awataka polisi kutowahangaisha wanabodaboda

Muhtasari

• Kiongozi wa ODM Raila Odinga amewataka maafisa wa polisi kukoma kuwahangaisha wanabodaboda bila sababu maalum.

• “Kuna kisa kilifanyika juzi huko Nairobi ambapo wanabodaboda walimshambulia mwanamke, lazima sote tukashifu kitendo hicho. Hata hivyo, tusikubali whudumu wote kuhangaishwa kwa makosa ya wachache,” alisema.

Fcebook, KWA HISANI
Fcebook, KWA HISANI
Image: Raila Odinga

Kiongozi wa ODM Raila Odinga amewataka maafisa wa polisi kukoma kuwahangaisha wanabodaboda bila sababu maalum.

Kauli ya Odinga inajiri siku chache baada ya rais Uhuru Kenyatta kutoa amri ya kuwapiga msasa waendesha bodaboda wote ili kunyoosha sekta hiyo.

Huku akishtumu vikali kitendo kilochofanyika katika barabara ya Wangari Maathai, Odinga alionya dhidi ya kuwahangaisha wanabodaboda waiokuwa na hatia.

Odinga alisema kwamba kuna idadi ndogo ya wahudumu hao ambao wanatoa picha mbaya kwa umma, huku akiwataka polisi kupambana zaidi ili kuhakikisha waliohusika wanakutana na mkono wa sheria.

“Kuna kisa kilifanyika juzi huko Nairobi ambapo wanabodaboda walimshambulia mwanamke, lazima sote tukashifu kitendo hicho. Hata hivyo, tusikubali whudumu wote kuhangaishwa kwa makosa ya wachache,” alisema.

Raila alikuwa akiyazungumza hayo Alhamisi katika kampeni za vuguvugu la Azimio kwenye eneo la Maua kaunti ya Meru ambapo alipigia debe muungano huo mbele ya uzinduzi wake rasmi ambao unaratibiwa kufanyika siku ya Jumapili.

Aliandamana na gavana wa kaunti ya Meru Kiraitu Murungi, waziri wa kilimo Peter Munya, mbunge wa zamani wa Gatanga Peter Kenneth na kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa Maoka Maore miongoni mwa wengine.