Shahidi: Niliahidiwa 10M kuondoa ushahidi dhidi ya Ruto ICC

Muhtasari

• Shahidi mmoja amekiri kuhongwa nyumba, kiwanja na kuahidiwa kiasi cha milioni 10 ili kuondoa ushahidi katika mahakama ya ICC dhidi ya naibu rais William Ruto.

• Alisema katika milioni kumi alizoahidiwa, alipokezwa kiasi cha milioni 2 pekee.

Kesi ya ukiukwaji mkubwa wa haki za kibinadamu kutokana na vurugu za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007-08, ambayo iliwahusisha Wakenya sita katika mahakama ya jinai ICC jijini Hague ilikamilika pasi na mtuhumiwa hata mmoja kati ya hao sita kuhukumiwa.

Kesi hiyo hivi majuzi ilichukua mkondo tofauti baada ya wakili Paul Gicheru kutajwa kuwa mshawishi mkubwa katika ushahidi dhidi ya naibu rais.

Katika matukio yanayoendelea hivi karibuni mahakamani humo, shahidi mmoja alisema alihongwa kiasi cha shilingi milioni kumi pesa za Kenya, kiwanja na nyumba iliyokuwa imemalizika kujengwa ili kuondoa Ushahidi wake dhidi ya William Ruto na aliyekuwa mwanahabari Joshua Arap Sang katika kesi hiyo ambayo pia wakili Paul Gicheru alitajwa.

Shahidi huyo ambaye jina lake lilibanwa kwa sababu za kiitifaki alisema alidokezewa na mashahidi wenzake kuhusu ofa hiyo ambayo tayari wao walikuwa wameshaipokea ili kuondoa ushahidi wao ICC.

Shahidi huyo aidha alisema katika kiasi cha milioni kumi alizoahidiwa kupata baada ya kuondoa mashtaka yake, alipokezwa tu kiasi cha milioni mbili pekee na mpaka sasa yungali bado kupokea milioni 8 zilizosalia.