Familia ya mwanafunzi aliyepigwa hadi kufariki shuleni Gatanga CMM yaandamana kwa ofisi ya rais wakidai haki

Muhtasari

• Maandamano hayo ya amani yalianzia katika bustani ya Jevanjee na kuelekea katika barabara ya Harambee Avenue jijini Nairobi, ambapo ofisi rasmi ya rais iko.

• Waandamanaji hao walimtaka rais Kenyatta kuingilia kati ili kuhakikisha haki ya marehemu mwanao inatendeka

Ebby Noelle Samuel, mwanafunzi wa Gatanga CCM aliyefariki kwa njia ya kutatanisha
Ebby Noelle Samuel, mwanafunzi wa Gatanga CCM aliyefariki kwa njia ya kutatanisha
Image: HISANI

Familia ya Ebby Noelle Samuel, mwanafunzi aliyefariki kwa njia ya kutatanisha katika bweni la shule ya Gatanga CMM mwezi Machi mwaka 2019 iliandamana Alhamis nje ya ofisi ya rais Uhuru Kenyatta ikitaka haki dhidi ya kinda wao kutendeka.

Maandamano hayo ya amani yalianzia katika bustani ya Jevanjee na kuelekea katika barabara ya Harambee Avenue jijini Nairobi, ambapo ofisi rasmi ya rais iko, huku wakimtaka rais Kenyatta kuingilia kati ili kuhakikisha haki ya marehemu mwanao inatendeka. Walikuwa wanateta kwamba miaka mitatu ni mingi sana ambapo haki imejeleweshwa.

Waandamanaji hao waliojumuisha wanafamilia wa mwanafunzi Ebby walikuwa wamebeba mabango yenye maandishi ya kutaka haki ifanyike ili waliosababisha kifo cha mwanao washtakiwe, ambao walidai wako huru miaka mitatu baadae tangu kifo cha mwanao shuleni.

Maandamanio hayo yalitiwa moto na taarifa ambayo kitengo cha ujasusi DCI walichapisha katika mitandao yao ya kijamii wakisema kwamba wamefanya uchunguzi upya na kupata kwamba mwanafunzi huyo, ambaye hadi kifo chake alikuwa na miaka 15 tu aliuawa na mmoja wa wasimamizi wakuu katika shule la upili ya Gatanga CMM.

DCI waliandika kwamba baada ya kuchukua ripoti kutoka kwa wanafunzi wenza ambao walishuhudia tukio la kupelekea kifo cha Ebby, sasa uchunguzi upo tayari na hivi karibuni watuhumiwa wote nyuma ya kifo chake watashtakiwa.

Mwanafunzi huyo alifariki bwenini kwa njia ya kutatanisha, wiki mbili tu baada kurejea shuleni kutoka likizo fupi kwa kile mashuhuda walisema aliadhibiwa vikali kwa kupamba na kuremba nywele yake, kinyume na kanuni za shule hiyo.