Kwendeni, siwezi kujiuzulu! Spika Muturi awaambia wabunge wa ODM na Jubilee

Muhtasari

• Spika Muturi amewazima wabunge ambao walimtaka ajiuzulu.

• Aliwataka kuanzisha mjadala wa kumng'atua mamlakani iwapo wanaamini katika uwezo wao.

Spika Justin Muturi wakati wa kikao na wanahabari katika Klabu ya United Kenya Nairobi Jumanne 11, Januari.
Spika Justin Muturi wakati wa kikao na wanahabari katika Klabu ya United Kenya Nairobi Jumanne 11, Januari.
Image: WILFRED NYANGARESI

Spika wa bunge la kitaifa, Justin Muturi amejitokeza na kujitetea vikali kwa kile wabunge wa vyama vya Jubilee na ODM walikitaja kuwa upendeleo katika vikao vya bunge kufuatia hatua yake ya hivi karibuni kujiunga na mrengo wa Kenya Kwanza unaoongozwa na naibu rais William Ruto, mbele ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Akihutubia kikao cha mchana cha bunge siku ya Alhamisi, Muturi aliwataka wabunge wanaohisi kwamba hana usawa kuwasilisha  mjadala wa kumng'atua mamlakani  kulingana na sheria.

Muturi alisema kwamba msimamo wake wa kisiasa haufai kamwe kuhusishwa na majukumu yake kama spika wa bunge la kitaifa, na kwamba atazidi kutekeleza majukumu yake kama ambavyo amekuwa akifanya miaka tisa iliyopita alipochukua hatamu hiyo.

Alijitetea akisema kwamba alipata nafasi hiyo kupitia chama cha kisiasa kama tu watangulizi wake, hivyo hapaswi kushtumiwa kwa sababu amebadilisha msimamo wake kisiasa.

"Mwaka 2018 niligombea nafasi ya spika kupitia chama cha Jubilee, na nyinyi wabunge ndo mlinipa majukumu hayo. Nafahamu tupo katika kipindi cha kisiasa, ila hamwezi kupinga usawa wangu katika bunge hili," Muturi alisema.

Aidha, alitoa mfano wa mataifa kama vile Uingereza, Marekani, Tanzania na Uganda ambapo maspika wa mabunge yao ni wabunge waliochaguliwa na wananchi na wanaegemea mirengo tofauti ya kisiasa.

Alishikilia kwamba hawezi kujiuzulu, huku akiwataka wabunge wanaogemea vyama vya Jubilee na ODM [vyote chini ya vuguvugu la Azimio la Umoja] kumng'atua mamlakani.