HELB yadai Kshs.8.45b za mikopo ambayo haijalipwa kwa miaka 10

Hadi Februari 2023, HELB ilikuwa na malimbikizi ya jumla ya Kshs. 60.3b ambayo sehemu yake ni Shilingi bilioni 8.45.

Muhtasari

• Mbunge wa Kilome Nzambia Thuddeus alishangaa kuwa kuna wabunge ambao wamekosa kulipa mkopo wa Helb.

Mkurugenzi Mtendaji wa Helb Charles Ringera wakati wa mahojiano mnamo Aprili 19, 2022. Picha: CHARLENE MALWA
Mkurugenzi Mtendaji wa Helb Charles Ringera wakati wa mahojiano mnamo Aprili 19, 2022. Picha: CHARLENE MALWA

Afisa mkuu mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) Charles Ringera amefichua kuwa bodi hiyo inadai jumla ya shilingi bilioni 8.45 kutoka kwa Wakenya waliohitimu zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Ringera aliwaambia wabunge kuwa hadi Februari 2023, bodi hiyo ilikuwa na malimbikizi ya jumla ya Shilingi bilioni 60.3 ambayo sehemu yake ni Shilingi bilioni 8.45.

“Mikopo mingi imekuwa ni ya wanafunzi ambao waliondoka nchini, hivyo tunashirikiana na mabalozi kujaribu kurejesha fedha hizo,” Ringera alisema.

Mkuu huyo wa Helb alikuwa akizungumza alipofika mbele ya Kamati ya Uwekezaji wa Umma kuhusu Elimu na Utawala Bora.

Alieleza kuwa kuna kipindi cha neema kuanza kulipa mkopo mara mwanafunzi anapohitimu.

“Tunawapa mwaka mmoja wapate ajira ndipo waanze kulipa mkopo huo lakini wengi wao wanaenda hadi miaka kumi,” alisema.

Mbunge wa Sotik Francis Sigei alimtaka bosi huyo kubuni mbinu za kuhakikisha mikopo hiyo inarejeshwa kwa wakati.

Sigei alieleza kuwa hatua hizo zinapaswa kuwa na adhabu ambayo itahakikisha uzingatiaji wa malipo.

"Lazima tuwe mifano mizuri kwa sababu ikianza na sisi wabunge kutolipa mikopo basi si vyema. Labda unaweza kuandika kwa Bunge la Kitaifa au Seneti kukusaidia kurejesha pesa hizo," Sigei alisema.

Mbunge wa Kilome Nzambia Thuddeus alisema inashangaza ikiwa kuna wabunge ambao wamekosa kulipa mkopo wa Helb.

Aliwakashifu wale ambao hawajalipa mkopo huo, akisema fedha hizo zinaweza kutumika kusaidia wanafunzi wanaohitaji katika vyuo vikuu.