Msajili wa vyama adinda kutekeleza mabadiliko ya Uhuru Jubilee

Mrengo wa Uhuru uliandaa Kongamano la NDC na kuidhinisha mabaadiliko makubwa ya uongozi wa chama wa Jubilee.

Muhtasari

• Mrengo wa Uhuru ulimtaja Jamleck Kamau kama mkurugenzi wa kitaifa wa uchaguzi kuchukua nafasi ya Kega.

Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu kusasishwa kwa uanachama wa vyama vya kisiasa baada ya makataa kuwasilisha wanachama wao katika ofisi zao mtaani Westlands mnamo Machi 29, 2022. Picha: MERCY MUMO
Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu kusasishwa kwa uanachama wa vyama vya kisiasa baada ya makataa kuwasilisha wanachama wao katika ofisi zao mtaani Westlands mnamo Machi 29, 2022. Picha: MERCY MUMO

Msajili wa Vyama vya Kisiasa amekataa kuthibitisha mabadiliko katika chama cha Jubilee ambayo yalifanywa na mrengo wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Mrengo wa Uhuru mnamo Mei 22 uliandaa Kongamano la Wajumbe wa Kitaifa na kuazimia kufanya mabadiliko makubwa ya uongozi wa chama ikiwa ni pamoja na kuwafukuza wanachama wa kundi pinzani.

NDC ilikuwa imeazimia kumfukuza aliyekuwa Mbunge wa Kieni Kanini Kega, ambaye amedai kutwaa nafasi ya Katibu Mkuu, Mbunge mteule Sabina Chege na Mweka Hazina wa Kitaifa Nelson Dzuya.

Hata hivyo, kwenye barua iliyoandikwa Mei 29 na kwa Kioni, msajili wa vyama alifahamisha kambi ya Uhuru kwamba ombi la kuthibitisha mabadiliko hayo lilikataliwa kwa sababu ya kushindwa kuwasilisha stakabadhi kamili.

Msajili wa vyama Anne Nderitu alisema Kioni hakuwasilisha orodha iliyotiwa sahihi ya na wajumbe waliohudhuria kongamano la NDC pamoja na nambari zao za vitambulisho ili afisi hiyo ibainishe kufanyika kwa NDC.

Alisema hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 8.1[1] na 23 cha katiba ya chama cha Jubilee mtawalia.

Ofisi hiyo pia ilisema Kioni hakuwasilisha nakili za kina za kongamano hilo ili kubaini mchakato huo na utaratibu wa uchaguzi. Ofisi ya msajili ilisema kwamba ni dondoo za nakili pekee ndizo zililowasilishwa.

“Kutokana na hayo hapo juu, hati zilizowasilishwa hazijakamilika,” barua hiyo iliyotiwa saini na Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu inaeleza.

Nderitu alisema Kioni alikuwa amewasilisha tu notisi ya kuitisha mkutano wa NDC wa Mei 22, 2023, notisi ya mabadiliko ya mahali na maazimio ya mkutano maalum wa NDC.

Wakati wa NDC, mrengo wa Uhuru ulimtaja Jamleck Kamau kama mkurugenzi wa kitaifa wa uchaguzi kuchukua nafasi ya Kega.

Chama pia kilimteua mwanablogu Pauline Njoroge kama naibu katibu mandalizi wake mpya huku Maison Leshomo akiwa mwenyekiti wa kitaifa wa ligi ya wanawake huku Katibu Mkuu wa zamani Saitoti Torome akiteuliwa kuwa mwenyekiti wa kitaifa kuchukua nafasi ya Nelson Dzuiya. Yasin Noor aliidhinishwa kama naibu katibu mkuu kuchukua nafasi ya Joshua Kutuny.

Katika mabadiliko hayo, chama kilikuwa kiwe na manaibu viongozi wanne wa chama. Wao ni Beatrice Gambo (mkakati), Maoka Maore (operesheni), Joseph Manje (mipango) na Kados Muiruri (uhamasishaji).

Wengine waliofurushwa ni waliokuwa wabunge walioteuliwa Naomi Shaban, Boniface Kinoti, Jimi Angwenyi, Mutava Musyimi na Rachel Nyamai.

TAFSIRI YA DAVIS OJIAMBO.