TSC yajipata pabaya baada ya kukata walimu ushuru wa nyumba, kinyume na maagizo ya mahakama

Misori alisema muungano huo hauungi mkono Mswada wa Fedha wa 2023 ambao ulizua taharuki miongoni mwa Wakenya.

Muhtasari

• Akelo Missori alisema wameona stakabadhi za malipo za walimu kadhaa zikionyesha kukatwa tozo.  

• Misori siku ya Jumatano alisema muungano huo utachukua hatua zote kulinda mapato na marupurupu ya walimu.

Katibu mkuu wa Kuppet Akello Misori.
Katibu mkuu wa Kuppet Akello Misori.
Image: HISANI

Muungano wa Walimu wa sekondari KUPPET umesema kwamba  utachukua hatua za kisheria dhidi ya Tume ya Kuajiri Walimu kwa kukatwa kwa ushuru wa Nyumba mwezi Januari licha ya mahakama kuharamisha ushuru huo.  

Katibu Mkuu wa Kuppet Akelo Misori siku ya Jumatano alisema muungano huo utachukua hatua zote kulinda mapato na marupurupu ya walimu.

 "Hii ni pamoja na kuanzisha kesi ya kupuuza maagizo ya mahakama dhidi ya TSC kuhusu suala hili la ushuru wa Ushuru wa Nyumba," alisema.  

Missori alisema wameona stakabadhi za malipo za walimu kadhaa zikionyesha kukatwa tozo.  

"Wanachama wengi kutoka kote nchini wametuonyesha hati zao za malipo na zote zinaonyesha Tume ilikata ushuru wa Nyumba kutoka kwa mishahara ya Januari 2024," Misori alisema.  

"Hii ni pamoja na kwamba kuna maagizo ya wazi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa kutangaza Ushuru wa Nyumba kuwa kinyume cha sheria na kinyume cha katiba."  

Misori alitaka kurejeshewa kwa pesa za ushuru wa nyumba zilizokatwa kutoka kwa mishahara ya walimu ya Januari.Kuppet ilisema TSC haiwezi kutoa kisingizio kwa kusema makato hayo yalifanyika kwa sababu walikuwa tayari wametayarisha orodha ya malipo.

 “Tumeona katika nchi hii walimu wanalipwa hata tarehe 17 mwezi unaofuata ikiwa kuna masuala madogo kwenye orodha ya mishahara, sasa suala kubwa kama hili ambapo Mahakama ya Rufaa imetoa amri, ingefaa mishahara yote kwa benki irejeshwe ili maagizo ya mahakama yazingatiwe," Misori alisema.  

Misori alisema hatua ya TSC kuwakata walimu ushuru huo harama inayonyesha kuwa tume hiyo ilikuwa tayari kukiuka sheria.  Alisema Kuppet inataka walimu warudishiwe pesa zilizokatwa mara moja. 

"Pia tumeomba uhakikisho kutoka kwa Tume kwamba itatii amri za mahakama kwenda mbele. Ikiwa ni pamoja na na hasa maagizo ya Ushuru wa Nyumba," alisema. 

Misori alisema muungano huo hauungi mkono kamwe Mswada wa Fedha wa 2023 ambao ulizua taharuki miongoni mwa Wakenya.