Mwili wa mwanariadha Kiptum umehamishiwa hadi makafani ya Eldoret

Hapo awali makumi ya wanariadha walifika katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Race Course kutazama mwili huo.

Muhtasari
  • Familia ya mwanariadha huyo iliuhamisha mwili kutoka Hospitali ya Race Course ambako ulipelekwa baada ya ajali ya Jumapili usiku iliyogharimu maisha yake kando ya barabara ya Eldoret-Kaptagat.
Kelvin Kiptum
Image: HISANI

Mwili wa mwanariadha Kelvin Kiptum umehamishiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Eldoret kusubiri mipango ya maziko.

Familia ya mwanariadha huyo iliuhamisha mwili kutoka Hospitali ya Race Course ambako ulipelekwa baada ya ajali ya Jumapili usiku iliyogharimu maisha yake kando ya barabara ya Eldoret-Kaptagat.

Mwili wa kocha wake pia ulihamishiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Eldoret.

Kiptum na kocha wake raia wa Rwanda Gervais Hakizimana walifariki katika ajali mbaya ya barabarani Jumapili usiku katika eneo la Kaptagat kando ya barabara ya Elgeyo Marakwet-Ravine.

Kiptum anasemekana kuwa ndiye aliyekuwa akiendesha gari lililokuwa likielekea Eldoret ajali hiyo ilipotokea.

Haya yanajiri huku Waziri wa Michezo Ababu Namwamba akitarajiwa kuzuru familia ya mwanariadha huyo katika kijiji cha Chepsamo huko Elgeyo Marakwet.

Hapo awali makumi ya wanariadha walifika katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Race Course kutazama mwili huo.

Miongoni mwa wanariadha wakuu katika chumba cha kuhifadhia maiti ni Vivian Cheruiyot, Moses Tanui, Geoffrey Kamworor na Daniel Komen.

"Ni msiba mkubwa kwamba tumempoteza mtu ambaye alikuwa na mustakabali mzuri", Cheruiyot alisema.