Jenerali Francis Ogolla kuzikwa Aprili 21 nyumbani kwake Alego Usonga

Mazishi hayo yanakuja mapema kwa sababu Jenerali Ogolla alikuwa ameacha wosia na maagizo kwamba azikwe ndani ya saa 72 baada ya kifo chake.

Muhtasari

• Ogolla aliaga pamoja na maafisa wengine wanane wa kijeshi Alhamisi alasiri katika ajali ya helikopta huko Marakwet Mashariki

• Walikuwa kwenye oparesheni ya amani katika maeneo mbalimbali ya eneo la North Rift.

• Miili ya Jenerali Ogolla na maafisa wengine tisa wa kijeshi ilisafirishwa hadi Nairobi Alhamisi usiku.

Miili ya wahasiriwa wa ajali ya ndege ya Jeshi la Ulinzi la Kenya iliokewa na maafisa wa kijeshi ilipowasili Nairobi Aprili 18, 2024. Picha: SCREEN GRAB
Miili ya wahasiriwa wa ajali ya ndege ya Jeshi la Ulinzi la Kenya iliokewa na maafisa wa kijeshi ilipowasili Nairobi Aprili 18, 2024. Picha: SCREEN GRAB

Marehemu Mkuu wa Majeshi (CDF) Francis Ogolla, 62, anatazamiwa kuzikwa nyumbani kwake Ng’iya huko Alego Usonga mnamo Aprili 21.

Hii ni kwa mujibu wa familia yake.

Viongozi pia walifichua kwamba mazishi hayo yanakuja mapema kwa sababu Jenerali Ogolla alikuwa ameacha wosia na maagizo kwamba azikwe ndani ya saa 72 baada ya kifo chake.

Duru zilisema kuwa wanajeshi wamearifiwa kuhusu wosia huo na kufanya kazi ndani ya muda uliopangwa ili kuhakikisha kuwa unaheshimiwa.

Maandalizi ya mazishi yamechukuliwa na serikali. Hii ni kwa sababu alifariki akiwa ofisini.

Miili ya Jenerali Ogolla na maafisa wengine tisa wa kijeshi ilisafirishwa hadi Nairobi Alhamisi usiku.

Miili hiyo ilipokelewa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta katika kituo cha kijeshi cha Embakasi ambapo ibada ilifanyika.

Kisha ilisafirishwa kwa ambulensi hadi Hospitali ya Forces Memorial kwa ajili ya kuhifadhiwa.

Siku ya Ijumaa, familia mbili za walioaga zilitembelea chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya utambuzi na uwezekano wa mazishi kulingana na taratibu za Kiislamu.

Chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana. Kikosi cha wataalam kilikwenda hadi eneo la tukio mnamo Ijumaa kuanza uchunguzi, maafisa walisema.

Ogolla aliaga pamoja na maafisa wengine wanane wa kijeshi Alhamisi alasiri katika ajali ya helikopta huko Marakwet Mashariki walipokuwa kwenye oparesheni ya amani katika maeneo mbalimbali ya eneo la North Rift.

Wengine wawili, hata hivyo, walinusurika katika tukio hilo la kusikitisha. Mabaki ya hao tisa yanahifadhiwa Nairobi.

Ogolla ameacha mjane na watoto wawili. Pia amewaacha binti-mkwe Muthoni Njenga na mjukuu Taji Mbarara.

Ogolla alizaliwa Februari 12, 1962, alijiunga na KDF kama Kadet  mnamo Mei 2, 1984 na akateuliwa kuwa luteni wa pili Mei 3, 1985, ambapo alitumwa Moi Airbase ambako alifunzwa kuwa rubani.

Wakati wa kazi yake katika KDF, Ogolla alishikilia nyadhifa mbali mbali.

Alikuwa Afisa Mkuu wa Kitengo cha Ndege cha Laikipia Air Base Tactical Flight mwaka katika 2007 na pia Kamanda wa Base Laikipa Air Base kutoka 2008 hadi 2014.

Alipopandishwa cheo na kuwa Brigedia mnamo Aprili 10, 2012, aliteuliwa kuwa Naibu Kamanda wa Jeshi la Anga na baadaye akapandishwa cheo na kuwa Meja Jenerali mnamo Julai 13, 2018 na kuteuliwa kuwa Kamanda wa Jeshi la Wanahewa la Kenya.

Julai 23, 2021, pia alipandishwa cheo na kuwa Luteni Jenerali na kuteuliwa kuwa Makamu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, nafasi ambayo aliishikilia hadi Aprili 28, 2023, alipopandishwa cheo na kuwa Jenerali na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi (CDF).

Kutokana na kujitolea kwake katika huduma, marehemu Ogolla alitunukiwa nishani kadhaa miongoni mwao Moran of the Golden Heart (MGH), Elder of The Burning Spars, (HSC) miongoni mwa zingine.