Raila Odinga amtembelea mjane wa Jenerali Francis Ogolla kumfariji

Aliandamana na viongozi wengine wakiwemo Kalonzo Musyoka, Martha Karua, Wycliffe Oparanya wakati wa ziara hiyo.

Muhtasari

•Gavana Orengo alifichua kuwa viongozi hao walifanya ziara hiyo ili kuwafariji familia na marafiki wa marehemu Jenerali Francis Ogolla.

•Picha zilizochapishwa na gavana Orengo zilionyesha viongozi hao wakiwapa pole familia na marafiki wa marehemu .

akimfariji Aieleen Ogolla.
Kingozi wa ODM Raila Odinga akimfariji Aieleen Ogolla.
Image: FACEBOOK// JAMES ORENGO

Kinara wa ODM Raila Amollo Odinga, mnamo Ijumaa asubuhi, alizuru nyumbani kwa marehemu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Francis Ogolla jijini Nairobi ambako alituma risala zake za rambirambi na kufariji familia.

Waziri Mkuu huyo wa zamani aliandamana na viongozi wengine wa Azimio la Umoja akiwemo gavana James Orengo, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, na aliyekuwa mgombea mwenza wa Azimio la Umoja Martha Karua wakati wa ziara hiyo.

Gavana wa Siaya James Orengo alifichua kuwa viongozi hao walifanya ziara hiyo ili kuwafariji familia na marafiki wa marehemu Jenerali Francis Ogolla.

"Leo asubuhi pamoja na Rt. Mhe. Raila Odinga, tuliwapa pole familia na marafiki wa marehemu Jenerali Francis Omondi Ogolla, EGH, EBS, HSC 'ndc' (K) 'psc' Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Francis Ogolla nyumbani kwake Nairobi,” gavana Orengo alisema kupitia Facebook.

Viongozi wengine waliokuwepo wakati wa ziara hiyo ni pamoja na naibu kiongozi wa ODM Wycliffe Oparanya, mbunge Millie Odhiambo, mbunge wa zamani wa Ndaragwa Jeremiah Kioni na aliyekuwa mbunge wa Murang’a Mwangi wa Iria miongoni mwa wengine.

Picha zilizochapishwa na gavana Orengo zilionyesha viongozi hao wakiwapa pole familia na marafiki wa marehemu kamanda wa vikosi vya ulinzi.

Hapo awali, Raila alieleza kusikitishwa kwake na kifo cha Jenerali Francis Omondi Ogolla, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi.

Jenerali Ogolla, pamoja na wanajeshi wengine kumi na moja, walihusika katika ajali mbaya ya helikopta katika eneo la Sindar, eneo la Kaben huko Elgeyo Marakwet, ambayo ilileta taharuki kote nchini.

Katika ujumbe wake wa kumuomboleza  Jenerali Ogolla, Raila Odinga alisema: “Siku mbaya kwa Kenya: Mke wangu Ida na mimi tumehuzunishwa sana na kifo cha Jenerali Francis Ogolla, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi."

Aliongeza, “Tunaungana na taifa katika kuomboleza kifo chake. Jenerali Ogolla alikuwa mzalendo wa kweli, mwanajeshi aliyepambwa sana na mtaalamu aliyekamilika ambaye alitumikia nchi yetu kwa kujitolea bila kuyumbayumba.”

Akielezea mshikamano na familia iliyojawa na huzuni, Raila aliongeza: “Mioyo yetu ni kwa familia yake, wafanyakazi wenzake katika KDF na taifa zima tunapoomboleza kifo huu mkubwa. Pia tunatuma rambirambi zetu kwa familia za timu ya KDF iliyoandamana na Jenerali Ogolla. Tunajua kwamba kwa wakati huu, maneno hayatatosha kufariji huzuni zenu kubwa. Tunawaombea Bwana awafariji na roho za wote waliofariki zipate amani ya milele.”