Mwanawe Muturi apotea baada ya kushukiwa kutekwa nyara Nairobi

AG Muturi alithibitisha kuwa familia bado haijampata Leslie.

Muhtasari
  • "Bado hajapatikana," AG Muturi alisema katika ujumbe Jumapili mwendo wa saa 11:30 asubuhi. Kesi hiyo imeripotiwa polisi.
Image: SCREENGRAB

Mwana wa Mwanasheria Mkuu (AG) Justin Muturi, Leslie Muturi, anashukiwa kuwa aidha alitekwa nyara au kukamatwa na watu wasiojulikana katika eneo la Lavington Nairobi.

AG Muturi alithibitisha kuwa familia bado haijampata Leslie.

"Bado hajapatikana," AG Muturi alisema katika ujumbe Jumapili mwendo wa saa 11:30 asubuhi. Kesi hiyo imeripotiwa polisi.

Mbunge wa Embakasi Magharibi Mark Mwenje alifichua kisa hicho usiku wa Jumamosi, Juni 22, akiwa amesimama kando ya gari la magurudumu manne ambalo Leslie alikuwa akitumia wakati akidaiwa kutekwa nyara.

Polisi wanasema hawajui ni nani aliyemchukua mwanamume huyo mwenye umri wa takriban miaka 40.

Leslie ni mfanyabiashara. Ripoti zinasema alikuwa kwenye klabu maarufu karibu na Dennis Pritt kabla ya kuondoka kwa gari lililokuwa limezuiwa mita chache mbele.

Alilazimika kutoka na kuingizwa kwenye gari tofauti ambalo liliondoka mara moja.

Chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana.

Katika video iliyosambaa mtandaoni Jumamosi jioni, Mwenje alidai kuwa Leslie, ambaye alimtaja kuwa rafiki yake, alitolewa nje ya gari lake na maafisa wa polisi kando ya barabara.

Mwenje alidai kuwa walikuwa wakiendesha magari tofauti pamoja na marafiki zao wengine katika eneo la Kilimani Nairobi wakati wanaodaiwa kuwa polisi walisimamisha gari la Leslie na kumchukua kwa Land Cruiser.

“Tulikuwa Kilimani, rafiki yangu Leslie Muturi, mwana wa AG Justin Muturi alikamatwa na polisi hapa barabarani. Mimi ndiye niliyemfuata, hili ni gari lake,” mbunge huyo alisema kwenye video hiyo.

SUV ya bluu ilikuwa kando ya barabara na milango yake na buti imefunguliwa.

“Kwa polisi waliomchukua tutakupata. Mwachieni sasa hivi, hatutalala mpaka tumpate. Tumefahamisha kila mtu jijini Nairobi,” asema kwenye video hiyo.

"Maafisa wanatuambia kuwa hawajui yuko wapi bado watu waliomchukua ni askari. Tulikuona ukiwa kwenye gari nyeupe aina ya Land Cruiser, ukiwa umevalia mavazi meusi. Tulikuona na tuna sahani zako."

Polisi walisema wanachunguza madai hayo.