Keter afichua sababu za kukamatwa kwake

“Nilipokamatwa, niliulizwa kuhusu uhusiano wangu na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta pamoja na naibu rais Rigathi Gachagua,”Keter alisema.

Muhtasari

• Alifichua kuwa polisi walikuwa wakimuuliza iwapo alikuwa na jukumu lolote katika usafirishaji haramu wa silaha kuelekea Congo kwani maafisa walikuwa wanamshuku.

• “Nilipokamatwa, niliulizwa kuhusu uhusiano wangu na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta pamoja na naibu rais Rigathi Gachagua,”Keter alisema.

• Keter alisisitiza kuwa sababu kuu ya kukamatwa kwake ilitokana na upinzani dhidi ya Mswada wa Fedha pamoja na maandamano ambayo yamekuwa yakijiri nchini.

Mbunge wa zamani wa Nandi Hills Alfred Keter
Image: HISANI

Mbunge wa zamani wa Nandi Hills Alfred Keter, mnamo Jumatatu, amesema kuwa alikuwa anapelelezwa na kuchunguzwa kuhusu uhusiano wake na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta vilevile Naibu wa Rais Rigathi Gachagua baada ya kukamatwa mnamo Jumapili.

Akizungumza kutoka kwenye Makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Keter alifichua kuwa polisi walikuwa wakimuuliza iwapo alikuwa na jukumu lolote katika usafirishaji haramu wa silaha kuelekea Congo kwani maafisa walikuwa wanamshuku.

“Nilipokamatwa, niliulizwa kuhusu uhusiano wangu na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta pamoja na naibu rais Rigathi Gachagua,”Keter alisema.

Hata hivyo, Keter alisisitiza kuwa sababu kuu ya kukamatwa kwake ilitokana na upinzani dhidi ya Mswada wa Fedha pamoja na maandamano ambayo yamekuwa yakijiri nchini.

Alieleza kwamba kukamatwa kwake kulikuwa kama mbinu ya vitisho kufuatia ukosoaji wake mkali wa serikali hapo awali.

“Wacha tufuate sheria na kanuni lakini msitutishie ili tunyamaze,” aliongezea.

Keter, vilevile aliishtaki serikali ya Kenya Kwanza kwa  kukosa kutimiza ahadi zao kwa wakenya ambazo walizisema siku za kampeni.

Mbunge huyo wa zamani aliishutumu serikali kwa kupotosha ukweli kwa watu wa Kenya ambao umeongeza tofauti miongoni mwa wakenya kuhusu jinsi wanavyohisi.

Hisia za mbunge huyo zinafuatia kukamatwa kwake kwa njia tata kiasi cha kuleta hamaki kwa wananchi kwani maafisa walilazimisha kukamatwa huko mnamo Jumapili huku wakimtoa ndani ya gari lake.

Fauka ya hayo, DCI walithibitisha kuwa kukamatwa kwake kulitokana na mbunge huyo wa zamani kujihusisha na usafirishaji haramu wa silaha vilevile uchochezi wa vurugu.

Rais Ruto akihojiwa na wanahabari mnamo Jumapili, alithibitisha kukamatwa kwa Keter akisema kuwa Keter alikuwa amekataa kutii amri za vyombo vya usalama.