Mbunge Didmus Barasa kujibu mashtaka ya mauaji mahakamani leo

Barasa alikaa wikendi nzima katika seli ya polisi baada ya kujisalimisha siku ya Ijumaa

Muhtasari

•Barasa alijisalimisha kwa polisi Alhamisi wiki iliyopita baada ya kitengo cha DCI kutangaza msako dhidi yake.

•Barasa alidai kwamba pia  yeye angetaka kujua ni kilichomuua Olunga kama mtu mwingine yeyote.

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa
Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa
Image: Facebook//DidmusBarasa

Mbunge mteule wa Kimilili Didmus Barasa anatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi leo. 

Barasa alikaa wikendi nzima ndani ya seli ya kituo cha polisi cha Bungoma baada ya kujisalimisha Ijumaa wiki iliyopita. Alichukua hatua ya kujisalimisha baada ya kitengo cha DCI kutangaza msako dhidi yake kwa tuhuma za mauaji ya msaidizi wa aliyekuwa mshindani wake wa karibu Brian Kahemba.

Kupitia taarifa, DCI ilisema kwamba imempa Barasa chini ya saa sita tu kujisalimisha la sivyo msako mkali dhidi yake ungeanzishwa na kumtia mbaroni.

"Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai inamuonya Mhe Didmus Barasa, ambaye amejificha baada ya mauaji ya kikatili ya Brian Olunga, kujisalimisha kwa kituo cha polisi kilicho karibu ndani ya saa 6 zijazo. Mhe Barasa, anasakwa kwa mauaji ya Brian, ambaye alimpiga risasi paji la uso na kumuua papo hapo, mnamo Jumanne, Agosti 8, eneo la Chebukwabi huko Kimilili, kaunti ya Bungoma," Sehemu ya ripoti hiyo ya DCI ilisema.

Baada ya  kujisalimisha, mbunge huyo alionekana kujitenga na tuhuma za mauaji ya Brian Olunga mnamo siku ya uchaguzi mkuu. 

Akizungumza na vyombo vya habari, Barasa alidai kwamba pia  yeye angetaka kujua ni kilichomuua Olunga kama mtu mwingine yeyote.

Mbunge huyo alisema anashirikiana na polisi katika uchunguzi wa suala hilo na kusema kwamba hakuwa amekimbilia nchi Jirani ya Uganda kama ambavyo fununu zilisema.

“Nilikwenda Nairobi kupata dhamana tarajiwa nikisubiri kukamatwa lakini nilipoona kwenye runinga kamanda wa polisi wa mkoa akinitaka nijisalimishe, niliendesha gari hadi eneo hili na niko tayari kutoa ushirikiano kwa polisi ili pia nijue nini kilimuua kijana huyo,” Barasa alisema.

Pia alidai kuwa Jumapili wiki jana, mmoja wa walinzi wake alivamiwa na kujeruhiwa vibaya na kwa yuko hospitalini akiendelea kupata nafuu.